• HABARI MPYA

    Wednesday, September 06, 2017

    YANGA KWENDA NJOMBE IJUMAA KUSAKA USHINDI WA KWANZA LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIKOSI cha Yanga kitaondoka Dar es Salaam Ijumaa kwenda Njombe kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Njombe Mji Jumapili Uwanja wa Saba Saba.
    Kipa Beno Kakolanya, kiungo Baruan Yahya na mshambuliaji Mrundi Amissi Tambwe hawatakuwemo kwa sababu ya majeruhi, lakini kocha Mzambia, George Lwandamina amefurahia kurejea kwa kiungo Pius Buswita na mshambuliaji, Mzambia Obrey Chirwa.
    Buswita alifungiwa na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kwa kosa la kusaini mikataba na timu mbili, nyingine Simba SC – lakini baada ya Yanga kuzungumza na kukubali kulipa fedha alizochukua mchezaji huyo kwa mahasimu wao, amesamehewa na amekubaliwa kuendelea na soka, wakati Chirwa alikuwa majeruhi.

    Kikosi kamili cha Yanga kinachosafiri kesho kwenda Njombe ni makipa; Youthe Rostand na Ramadhan Kabwili, mabeki Hassan Kessy, Juma Abdul, Gardiel Michael, Mwinyi Mngwali, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Pato Ngonyani, Andrew Vincent ‘Dante’ na Abdallah Shaibu ‘Ninja’.
    Viungo Pius Buswita, Juma Mahadhi, Thabani Kamusoko, Papy Kabamba Tshishimbi, Said Juma ‘Makapu’, Said Mussa, Raphael Daudi, Geoffrey Mwashiuya, Emmanuel Martin na Yussuf Mhilu wakati washambuliaji ni Obrey Chirwa, Donald Ngoma, Ibrahim Hajib na Matheo Anthony. 
    Yanga itakwenda Njombe ikiwa na kumbukumbu ya kucheza mechi mbili bila kushinda, kwanza ikifungwa kwa penalti 5-4 na Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii Agosti 23, baada ya sare ya 0-0 Uwanja wa Taifa, kabla ya kulazimishwa sare ya 0-0 na Lipuli ya Iringa Agosti 27 Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu.
    Kocha Lwandamina anakabiliwa na shinikizo la kushinda mchezo huo, ili kurejesha imani kwa wapenzi wa timu hiyo kwamba wana timu ya kushindani mataji.
    Na hiyo ni kutokana na imani kwamba msimu huu utakuwa wa ushindani zaidi baada ya mahasimu wao, Simba kufanya usajili mzuri kufuatia kurejea kwa mfadhili wake wa zamani, Mohammed Dewji.
    Lakini pia Azam FC nayo imeonekana kujiimarisha kwa usajili na maandalizi mazuri, huku Singida United iliyopanda ikiwa timu nyingine inayoleta presha kwa vigogo baada ya usajili na maandalizi mazuri pia chini ya kocha wa zamani wa Yanga, Mholanzi, Hans van der Pluijm.
    Hiyo ni mbali ya ushindani wa kawaida uliozoeleka kutoka kwa timu kama Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Mbao FC, Prisons, hata Mwadui FC na Stand United.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA KWENDA NJOMBE IJUMAA KUSAKA USHINDI WA KWANZA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top