• HABARI MPYA

    Saturday, September 02, 2017

    TAIFA STARS YARUDI ‘SHAMBA LA BIBI; BAADA YA MIAKA 11

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo inateremka kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kumenyana na Botswana ‘The Zebras’ katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa.
    Huo utakuwa ni mchezo wa 12 kwa kocha Salum Shabaaban Mayanga tangu ampokee mzalendo mwenzake, Charles Boniface Mkwasa Machi mwaka huu, akiwa ameshinda mechi tano, sare tano na kufungwa moja.
    Katika mchezo wa leo, kocha Mayanga amewapata wachezaji wake wote wanaocheza nje aliowaita kasoro mmoja tu, mshambuliaji Orgenes Mollel wa FC Famalicao ya Ureno ambaye amenyimwa ruhusa na klabu yake kutokana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutofuata taratibu za kumuita.
    Lakini wengine wote, beki Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, winga Simon Msuva wa Difaa Hassan El –Jadida ya Morocco, Elias Maguli wa Dhofar FC ya Oman, Farid Mussa wa CD Tenerife ya Hispania na Nahodha Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji wamekuja.
    Mara ya mwisho Taifa Stars kucheza Uwanja wa Uhuru, ilikuwa ni Jumamosi ya Desemba 9, mwaka 2006 iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), wafungaji Gaudence Mwaikimba na Nizar Khalfan.
    Kutoka hapo, Stars ikiwa chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo ikaenda kuweka kambi ya mwezi mmoja Brazil kabla ya kwenda kufungwa 4-0 na Senegal Machi 24, mwaka 2007 kwenye mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mjini Dakar.
    Baada ya mchezo huo, Taifa Stars ikaenda kulazimishwa sare ya 1-1 na Uganda Mei 26, mwaka 2007 mjini Uwanja wa Nakivubo mjini Kampala kabla ya kwenda kucheza mechi ya kwanza Uwanja wa mpya wa Taifa, Septemba 1, mwaka 2007, bao pekee la Abdi Kassim ‘Babi’ likiipa Taifa Stars ushindi wa 1-0.
    Takriban miaka 11 baadaye, Stars inarudi Shamba la Bibi kwa mchezo na Botswana.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS YARUDI ‘SHAMBA LA BIBI; BAADA YA MIAKA 11 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top