• HABARI MPYA

  Saturday, September 02, 2017

  SAID MAULID: NI VIZURI KUBORESHA DARAJA LA KWANZA KULIKO KUONGEZA TIMU LIGI KUU

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MCHEZAJI wa zamani wa Simba na Yanga, Said Maulid ‘SMG’ amesema kwamba kuongeza timu katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara haitakuwa na maana kama kuimarisha Ligi Daraja la Kwanza ili iwe ya ushindani zaidi na kuzalisha wachezaji bora.
  Maulid amesema hayo leo katika mahojiano maalum na Bin Zubeiry Sports – Online kufuatia tamko la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwamba litapandisha idadi ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu msimu ujao wa 2018/19 kutoka 16 za sasa hadi 20.
  “Mimi ninachoona, tunapaswa kuimarisha Ligi Daraja la Kwanza, iwe ligi kubwa na yenye ushindani zaidi. Tukifanya hivyo itatusaidia kuzalisha nyota wa kiwango kizuri kuanzia chini,”amesema.
  Said Maulid ‘SMG’ amesema vyema kuboresha Ligi Daraja la Kwanza kuliko kuongeza timu katika Ligi Kuu

  Maulid amesema kwa mfumo wa sasa, Ligi Daraja la Kwanza imekuwa ya ovyo mno na haina ushindani wowote, ndiyo maana timu inayopanda Ligi Kuu inafumua kikosi na kusajili karibu wachezaji wote wapya.
  Amesema hiyo ni tofauti na miaka ya nyuma, wakati ambao timu zilipanda kutoka Daraja la Kwanza na vikosi vyao vile vile ikaingia navyo Ligi Kuu na kwua tishio.
  “Historia inaonyesha timu ya Tukuyu Stars ilipanda na wachezaji wake na ikaenda kuwa bingwa wa Ligi Kuu mwaka 1986. Lakini timu nyingine nakumbuka zilikuwa zinapanda Ligi Kuu na wachezaji wake na zinakuwa tishio kama Bandari Mtwara,” amesema.
  Said amesema hata yeye alichukuliwa timu ya taifa akiwa anacheza timu ya Daraja la Pili, Reli Kigoma mwaka 1999 na moja kwa moja akasajiliwa na klabu ya Simba na akafanikiwa kuwa mchezaji mkubwa katika soka ya Tanzania.   
  “Na hata hii ya kuongeza timu hadi 20, haina maana kama timu zitakuwa dhaifu, nakumbuka mwaka 2004 Ligi Kuu ilikuwa na timu 20, lakini baadaye zilipunguzwa kwa sababu timu nyingi zilikuwa hazina uwezo zinafungwa magoli mengi,”amesema.
  Agosti 22, mwaka huu Kamati ya Utendaji ya TFF ilifanya marekebisho ya Kanuni za Ligi Daraja la Kwanza inayotarajiwa kuanza Septemba 16, mwaka huu na sasa timu zitakazoshuka daraja msimu ujao kutoka Ligi Kuu ya Vodacom zitakuwa mbili hivyo kubaki 14 na ili kufikia timu 20, timu sita (6) za Ligi Daraja la Kwanza zitapanda daraja.
  Kwa mujibu wa utaratibu wa Ligi Daraja la Kwanza, timu, ina maana kwamba msimu huu timu mbili zitapanda kutoka katika kila kundi katika ligi hiyo ambayo inatarajiwa kuanza Septemba 16, mwaka huu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAID MAULID: NI VIZURI KUBORESHA DARAJA LA KWANZA KULIKO KUONGEZA TIMU LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top