• HABARI MPYA

    Thursday, April 02, 2015

    YANGA SC YAENDA NA ASKARI 18 BULAWAYO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    YANGA SC itaondoka kikosi cha wachezaji 18 kesho kwenda Bulawayo, Zimbabwe kwa ajili ya mchezo wa marudiano hatua ya 32 Bora Kombe la Shirikisho Afrika.
    Katika msafara huo, watakosekana wachezaji sita kwa sababu tofauti- ambao ni kipa wa tatu Alphonce Matogo, beki Edward Charles, viungo Andrey Coutinho, Hassan Dilunga na washambuliaji Kpah Sherman na Jerry Tegete.
    Sherman, Coutinho na Jerry Tegete ni majeruhi, wakati wengine wameachwa tu kwa sababu hawamo kwenye programu ya mchezo huo.

    Wachezaji wanaotarajiwa kuondoka kesho ni makipa Deo Munishi ‘Dida’ na Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Juma Abdul, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Pato Ngonyani, Rajab Zahir, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondan.
    Viungo ni Salum Telela, Said Juma, Nizar Khalfan, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Mrisho Ngassa na washambuliaji Danny Mrwanda, Amisi Tambwe na Hussein Javu.
    Benchi la Ufundi litaongozwa na Kocha Mkuu, Mholanzi, Hans van der Pluijm, Msaidizi wake Charles Boniface Mkwasa, kocha wa makipa Juma Pondamali, Meneja Hafidh Saleh, Daktari Sufiani Juma, mtunza vifaa, Mahmoud Omar ‘Mpogolo’ na Mchua misuli Jacob Onyango.
    Timu hiyo inatarajiwa kuondoka kuanzia Saa 4:00 asubuhi kwa ndege maalum ya kukodi ya serikali na itafikia katika hoteli ya Rainbow na jioni itakwenda kufanya mazoezi ya kuuzoea Uwanja wa Mandava.
    Platinum watatakiwa kuupanda mlima kama wanataka kusonga mbele michuano hiyo ya pili kwa ukubwa kwa klabu barani, kufuatia awali kufungwa 5-1 na Yanga.
    Ushindi wa mabao 4-0 Uwanja wa Mandava keshokutwa utaifanya timu hiyo yenye maskani yake Zvishavane iitoe Yanga SC kwa faida ya bao la ugenini.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YAENDA NA ASKARI 18 BULAWAYO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top