• HABARI MPYA

    Tuesday, April 07, 2015

    MICHO: TANZANIA WANA KIKOSI KIZURI CHA CHAN, LAKINI NAJUA NITAWATOAJE

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mserbia wa Uganda, Milutin Sredojevic ‘Micho’ (pichani kushoto) amesema kwamba Tanzania itakuwa na kikosi imara sana cha kufuzu Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, lakini atajitajidi awatoe.
    Tanzania ‘Taifa Stars, itaanza na Uganda katika Raundi ya kwanza kufuzu CHAN, ambayo Fainali zake zitafanyika nchini Rwanda mwaka 2016.
    Mechi za kwanza zitachezwa kati ya Juni 19, 20 na 21 mwaka huu na marudiano yatakuwa kati ya Julai 3, 4 na 5 mwaka 2015 na Micho amesema ni ‘babu kubwa’ Tanzania na Uganda zinakutana kwa mara ya tatu kwa mechi za kufuzu tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo mwaka 2009.
    “Tunaiheshimu timu ya Tanzania ya CHAN, asilimia 95 ya wachezaji wake waliocheza mechi za kufuzu AFCON (Fainali za Mataifa ya Afrika) wanatoka kwenye timu tatu kubwa za Tanzania, Yanga, Azam SC na Simba na timu nyingine za hapo hapo Tanzania,”.
    “Hii inakuwa changamoto kubwa kwa Uganda kucheza na Tanzania kubwa. Lakini tunajenga hali ya kujiamini kutokana na ukweli kwamba, tukiwa na timu mpya ya CHAN tutawajenga wachezaji wetu kupambana na timu yenye uzoefu,”.  Wachezaji wangu wengi waliocheza CHAN awali, kwa sasa wanacheza soka ya kulipwa nje,”amesema Micho. 
    Micho akizungumza na Brian Majwega kulia, mmoja wa wachezaji walioiongoza Uganda kuitoa Tanzania katika kufuzu CHAN iliyopita, ambaye kwa saa anachezea Azam FC ya Dar es Salaam  
    Kocha huyo wa zamani wa Yanga SC, amesema kwamba anatarajia ushindani mkubwa katika mechi zote mbili, ya nyumbani Uganda na ugenini Tanzania na atafanya kila kinachowezekana kuhakikisha anaitoa timu ya Mholanzi, Mart Nooij.
    “Kuna mambo madogo madogo yanatupa kipaumbele (Uganda), basi tutayatumia hayo kuhakikisha tunaitoa Tanzania,”amesema Micho.
    Baada ya ratiba ya michuano hiyo iliyopangwa juzi mjini Cairo, Misri mshindi kati ya Tanzania na Uganda, atakutana na Sudan iliyofuzu moja kwa moja Raundi ya Kwanza.
    Katika droo hiyo iliyoongozwa na Katibu wa CAF, Hicham El Amrani aliyesaidiwa na Makamu wa Pili wa Rais wa CAF, Almamy Kabele Camara, ambaye ni Rais wa Kamati ya Maandalizi ya CHAN, Kenya itaanza na Ethiopia na Burundi itacheza na Djibouti kwa kanda ya Afrika Mashariki na Kati.
    Mshindi kati ya Kenya na Ethiopia atakutana na mshindi kati ya Burundi na Djibouti katika Raundi ya Kwanza.
    Mechi za kwanza za hatua hiyo zitachezwa kati ya Oktoba 16, 17 na 18 na marudiano kati ya Oktoba 23, 24 na 25 mwaka huu na washindi wa mechi hizo za Raundi ya Kwanza watafuzu moja kwa moja kwenye fainali hizo, wakiungana na wenyeji Rwanda pamoja na nchi za kanda nyingine.
    Tanzania iliitoa Uganda katika kufuzu CHAN 2009, ikiifunga 2-0 Mwanza na kwenda kulazimisha sare ya 1-1 Kampala, wakati kufuzu CHAN iliyopita, The Cranes iliifunga 1-0 Taifa Stars Dar es Salaam na 3-1 Kampala.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MICHO: TANZANIA WANA KIKOSI KIZURI CHA CHAN, LAKINI NAJUA NITAWATOAJE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top