• HABARI MPYA

  Monday, December 15, 2014

  YANGA SC WATAKA KUKATA MBRAZIL MMOJA, KIIZA...

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  WAKATI dirisha dogo la usajili linafungwa leo Saa 6:00 usiku, klabu ya Yanga SC inafikiria kumuacha Mbrazil mmoja kati ya Andrey Coutinho na Emilson de Oliviera Rogue, ili ama imrejeshe Mganda Hamisi Kiiza, au isajili mchezaji mwingine.
  Kiiza aliondoka kambini siku moja kabla ya mechi ya Nani Mtani Jembe ambayo Yanga SC ilifungwa 2-0 na Simba SC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kufuatia taarifa kwamba yeye ndiye atakayekatwa baada ya kusajiliwa Mliberia, Kpah Sean Sherman.
  Lakini uongozi wa Yanga SC unasistiza bado haujamuacha mchezaji huyo, ingawa taarifa zinasema alikwenda kujaribu kujiunga na mahasimu, Simba SC ambako alikwama kwa sababu hakuwa na barua ya kutemwa na bado ana Mkataba na mwajiri wake wa sasa.
  Andrey Coutinho hajavutia Yanga SC baada ya mechi 11 akifunga mabao matatu

  Kutemwa Kiiza ni pendekezo la kocha Mbrazil wa Yanga SC, Marcio Maximo, lakini uongozi wa klabu hiyo hadi sasa haujaafiki.
  Yanga SC hawajaridhishwa na uwezo wa Coutinho, aliyeichezea klabu hiyo mechi 11 na kuifungia mabao matatu, lakini kikwazo ni Mkataba wake mrefu ambao utawalazimu kumlipa fedha nyingi wakimuacha.  
  Wakala aliyemleta Mliberia, Sherman ambaye amewavutia wana Yanga wengi baada ya kuichezea klabu hiyo kwa mara ya kwanza juzi, amewahakikishia viongozi wa klabu hiyo anaweza kuwapatia mchezaji mwingine mzuri ndani ya Saa 12 na kukamilisha usajili wake wote.
  Katika dirisha dogo, Yanga SC imesajili wachezaji watatu mbali na Mbrazil Emerson na Mliberia Sherman, mwingine ni mzalendo mshambuliaji Dan Mrwanda.
  Kwa upande wa Simba SC, jana imewasainisha mikataba wachezaji wawili wa kimataifa wa Uganda, beki Juuko Murushid na mshambuliaji Simon ‘Sam’ Sserunkuma, siku moja baada ya kuisaidia timu hiyo kushinda 2-0 dhidi ya Yanga SC.
  Amisi Tambwe anaondoka Simba SC licha ya kuwa mfungaji bora msimu uliopita

  Wawili hao wote walicheza juzi mechi ya Nani Mtani Jembe, Simba SC ikiwafunga mahasimu wao wa jadi, Yanga SC 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mabao ya kipindi cha kwanza ya Awadh Juma na Elias Maguri.
  Wawili hao wanachukua nafasi za Warundi kiungo Pierre Kwizera na mshambuliaji Amisi Tambwe wanaotemwa na sasa wanaungana na Waganda wenzao, beki Joseph Owino na washambuliaji Dan Sserunkuma na Emmanuel Okwi kukamilisha idadi ya wachezaji watano wa kigeni kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu.
  Tambwe aliyejiunga na Simba SC msimu uliopita pamoja na Mrundi mwenzake, Gilbert Kaze aliyetemwa Desemba mwaka jana, anaondoka Msimbazi baada ya kuichezea timu hiyo mechi 43 na kuifungia mabao 26.
  Tambwe ndiye aliyeibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Bara msimu uliopita- baada ya kuivutia Simba SC akiichezea Vital’O ya Burundi katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu Kombe la Kagame nchini Sudan mwaka jana na kuiwezesha kutwaa taji hilo naye akiwa mfungaji bora.
  Pierre Kwizera aliyesajiliwa kutoka Ivory Coast mwanzoni mwa msimu, hadi anaondoka amecheza mechi 14 bila kufunga bao.
  Kwa upande wa Azam FC, imeongeza wachezaji watatu karika dirisha dogo, ambao ni beki Serge Wawa Pascal raia wa Ivory Coast aliyekuwa anacheza El Merreikh ya Sudan, winga wa Uganda Brian Majwega aliyekuwa anacheza KCCA ya Kampala na kiungo mzalendo, Amri Kiemba aliyetua kutoka Simba SC.
  Serge Wawa Paacal amesajiliwa Azam FC kutoka El Merreikh ya Sudan

  Wawa na Majwega wanaungana na pacha wa Ivory Coast, Kipre Tchetche na Kipre Balou na Mrundi, Didier Kavumbangu kukamilisha idadi ya wachezaji watano wa kigeni Azam FC, huku Leonel Saint- Preux wa Haiti akitemwa.
  Vinara wa Ligi Kuu hadi sasa, Mtibwa Sugar wao wameimarisha kikosi chao kwa kumsajili mkongwe, Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, kiungo Henry Joseph Shindika aliyewika Simba SC kabla ya kwenda Norway.
  Zaidi ya hapo, Wakata Miwa hao wa Manungu wameendelea na utamaduni wao wa kupandisha wachezaji chipukizi kutoka timu yao ya vijana. Mbeya City imeimarisha safu yake ya ulinzi kwa kumsajili beki mkongwe, Juma Said Nyosso, wakati Coastal Union imemsajili kiungo Abdulhalim Humud ‘Gaucho’.
  Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linatarajiwa kutoa orodha kamili ya wachezaji waliongia katika klabu zote kwenye dirisha hili dogo baada ya Saa 6:00 usiku wa leo.     
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC WATAKA KUKATA MBRAZIL MMOJA, KIIZA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top