• HABARI MPYA

  Friday, December 05, 2014

  TUZO ZA WANAMICHEZO BORA TANZANIA, MDHAMINI MWINGINE AMWAGA MILIONI 30

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAMPUNI ya, Selcom Wireless imechangia kiasi cha Sh Milioni 30 kuelekea Tuzo za Wanamichezo Bora nchini za Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) Ijumaa wiki ijayo katika ukumni wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
  Zaidi ya wanamichezo 47 wanatarajiwa kupewa tuzo Desemba 12 na akizungumza wakati anatoa fedha hizo, Meneja Biashara na Masoko, Juma Mgori amesema kwamba mchango huo ni sehemu ya kampuni yao kujihusisha mambo ya kijamii.
  Mgori amesema kwamba wanajivunia sana kuwa miongoni mwa wadhamini katika tuzo ambazo zitamtoa rasmi mwanamichezo bora wa msimu wa 2013/14. 

  Meneja  Biashara, ukuzaji na Masoko wa kampuni ya Selcom Wireless, Juma Mgori (Katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na udhamini wa Tuzo za wanamichezo bora za Chama cha waandishi wa habari za michezo nchini (Taswa). Kampuni hiyo imetoa udhamini wa Sh Milioni 30. Kushoto ni Gallus Runyeta ambaye ni Meneja Miradi wa kampuni hiyo na kulia ni Mwenyekiti wa Taswa, Juma Pinto.

  Wadhamini wengine ni Said Salim Bakhresa & Co Ltd , IPTL, mifuko ya hifadhi ya jamii, PSPF na NSSF.
  Alisema kuwa  huo ni mwanzo tu wa kushirikiana na Taswa kwani wameingia katika dakika za mwisho kutokana na kujali umuhimu wa michezo nchini na kuona bora kutoa mchango wao.
  “Kama unavyojua, kampuni yetu inashughulikia malipo ya kielektoniki kwa taasisi za fedha 30 na tuna vituo vya malipo (Point of Services) zaidi ya 8,000, sisi ndiyo tunayoiwezesha jamii katika kila kona ya nchi yetu, hivyo mwakani tutaingia kwa nguvu zaidi,” alisema Mgori.
  Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taswa, Juma Pinto aliipongeza kampuni hiyo kwa kuwasaidia na pia kuendelea kuziomba kampuni nyingine na wadau wa michezo nchini kuwasaidia pamoja na muda kukaribia mwishoni.
  “Naishukuru Selcom Wireless na wadhamini wengine kwa kutoa ‘ubani’ wao katika shughuli hii muhimu, bado ni tunahitaji msaada na tunaamini kuwa wadau wengine watajitokeza kutusaidia,” alisema Pinto.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TUZO ZA WANAMICHEZO BORA TANZANIA, MDHAMINI MWINGINE AMWAGA MILIONI 30 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top