• HABARI MPYA

  Sunday, December 14, 2014

  SIMBA SC YAWATUPIA VIRAGO TAMBWE KWIZERA, YAWAPA MIKATABA ‘MINONO’ SAM SSERUNKUMA NA JUUKO

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imewasainisha mikataba wachezaji wawili wa kimataifa wa Uganda, beki Juuko Murushid na mshambuliaji Simon ‘Sam’ Sserunkuma, siku moja baada ya kuisaidia timu hiyo kushinda 2-0 dhidi ya Yanga SC.
  Wawili hao wote walicheza jana mechi ya Nani Mtani Jembe, Simba SC ikiwafunga mahasimu wao wa jadi, Yanga SC 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mabao ya kipindi cha kwanza ya Awadh Juma na Elias Maguri.
  Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba Murushid amesaini miaka mitatu, wakati Simon amesaini miaka miwili.
  Kusajiliwa kwa Waganda hao wawili, maana yake Warundi kiungo Pierre Kwizera na mshambuliaji Amisi Tambwe wanatemwa rasmi katika klabu hiyo.
  Makamu Rais wa Simba SC, Geoffrey Nyange 'Kaburu' kushoto akimkabidhi jezi namba sita Sam Sserunkuma


  Kaburu akimkabidhi jezi Juuko

  Simba SC inalazimika kuwatema Warundi hao ili kukidhi matakwa ya kanuni ya Usajili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ya wachezaji watano wa kigeni.
  Murushid na Sserunkuma wanaungana na Waganda wenzao, beki Joseph Owino na washambuliaji Dan Sserunkuma na Emmanuel Okwi kukamilisha idadi ya wachezaji watano wa kigeni.
  Tambwe aliyejiunga na Simba SC msimu uliopita pamoja na Mrundi mwenzake, Gilbert Kaze aliyetemwa Desemba mwaka jana, anaondoka Msimbazi baada ya kuichezea timu hiyo mechi 43 na kuifungia mabao 26.
  Tambwe ndiye aliyeibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Bara msimu uliopita- baada ya kuivutia Simba SC akiichezea Vital’O ya Burundi katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu Kombe la Kagame nchini Sudan mwaka jana na kuiwezesha kutwaa taji hilo naye akiwa mfungaji bora.
  Pierre Kwizera aliyesajiliwa kutoka Ivory Coast mwanzoni mwa msimu, hadi anaondoka amecheza mechi 14 bila kufunga bao.
  Juuko akisaini Mkataba wa Simba SC
  Sam Sserunkuma akisaini Mkataba wa Simba SC
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAWATUPIA VIRAGO TAMBWE KWIZERA, YAWAPA MIKATABA ‘MINONO’ SAM SSERUNKUMA NA JUUKO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top