• HABARI MPYA

  Friday, December 05, 2014

  SIMBA NA YANGA ZOTE ZAPANGWA KOMBE LA MAPINDZI, MICHUANO KUANZA JANUARI 1

  Na Salum Vuai, ZANZIBAR
  MASHINDANO ya Kombe la Mapinduzi 2015 yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi katika Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar Januari 1, mwakani, vigogo Simba na Yanga wakipangwa kushiriki.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa VIP, Uwanja wa Amaan, Zanzibar leo mchana, Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Kassim Haji Salum, alisema michuano hiyo itashirikisha timu 11 kutoka Zanzibar, Tanzania Bara na Pemba.
  Kassim alizitaja timu hizo kuwa ni mabingwa watetezi KCC ya Uganda, AFC Leopards kutoka Kenya, Yanga SC, Simba SC na Azam FC zote kutoka Dar es Salaam.
  Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein akimkabidhi Kombe, Nahodha wa KCCA, baada ya kutwaa taji hilo Januari mwaka huu Zanzibar

  Timu nyengine ni Mtibwa Sugar ya Morogoro, mabingwa wa soka Zanzibar KMKM, makamu bingwa Polisi, JKU, Mtende Rangers pamoja na timu ngeni kwenye Ligi Kuu ya Zanzibar Shaba FC kutoka wilaya ndogo Kojani kisiwani Pemba.  
  Katibu huyo alisema tayari timu zote zimeshapelekewa mialiko, na kwamba zinatakiwa kuthibitisha ushiriki wao si zaidi ya Disemba 15, mwaka huu.
  Alifahamisha kuwa mechi zote zitachezwa katika uwanja wa Amaan na kuongeza kuwa ratiba itapangwa mara tu baada ya timu kuthibitisha kushiriki.
  Kassim alisema fainali ya mashindano hayo itafanyika Januari 13, 2014 katika uwanja wa Amaan.
  Hata hivyo, alisema utaratibu huo unaweza kubadilika kidogo kutegemea na wapi kilele cha sherehe za Mapinduzi yanayotimiza miaka 51 mwakani, zitafanyika kati ya Unguja na Pemba.  
  Kuhusu wadhamini, alifahamisha kuwa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, imeahidi kuyasimamia kwa hali na mali kuhakikisha yanafanyika kwa ufanisi.
  Kassim alieleza kuwa, michuano hiyo inaratibiwa kwa pamoja kamati ya ZFA na Kamati ya Kombe la Mapinduzi iliyo chini ya ulezi wa Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA NA YANGA ZOTE ZAPANGWA KOMBE LA MAPINDZI, MICHUANO KUANZA JANUARI 1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top