• HABARI MPYA

  Sunday, December 07, 2014

  SIJUI YANGA SC WANAMCHUKULIAJE MAXIMO KWA SASA

  NADHANI Yanga SC ndiyo inayoongoza kuandikwa katika safu yangu hii. Na bahati mbaya sana, aghalabu nimekuwa nikiandika heko kwao, zaidi ni kuelezea mapungufu yao.
  Wengine wanadhani nafanya hivyo kwa sababu ninaichukia, na wengine wanafikiri nafanya hivyo kwa sababu ninaipenda sana.
  Huwezi kuzuia mitazamo na dhana za watu juu ya jambo au kitu chochote- lakini pia kwa namna yoyote uhalisia utabaki pale pale juu ya kile ninachoandika.
  Nashukuru, mara nyingi wana Yanga wenyewe wamekuwa wakikubali juu ya ninayoandika - ila tu labda wanatamani ningeandika barua ya maoni na kuipeleka klabuni kwao kuliko kuandika hapa.
  Lakini huo siyo mwongozo wa kitaalama. Tutaendelea kuambiana hapa hapa, ila ukweli tu, bila kuogopana, wenye kununa, wanune na wavimbe hadi wapasuke. Mimi nafikisha ujumbe kwa manufaa ya klabu yao wenyewe.
  Nilikuwa miongoni mwa mashabiki wachache waliojitokeza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kushuhudia mchezo wa kirafiki baina ya timu hiyo dhidi ya Express ‘Tai Wekundu’ wa Kampala, Uganda jana.
  Pongezi kwao Yanga SC kwa ushindi wa 1-0 jana, siku moja tu baada ya wapinzani wao, Simba SC kulazimishwa sare ya 0-0 na Waganda hao hapo hapo Taifa.

  Bila shaka, wapenzi wengi wa Yanga SC kati ya wachache waliojitokeza walitarajia kumuona kiungo wao mpya, Mbrazil Emerson de Oliviera Roque akicheza kiungo cha chini.
  Lakini kwa bahati mbaya, Mbrazil huyo aliyesaini Mkataba wa mwaka mmoja wiki iliyopita baada ya majaribio ya siku tatu, hata benchi hakuwepo.
  Ilikuwa ni fursa nzuri kwake Emerson kujitambulisha na kuitambulisha soka yake kwa wapenzi wa timu yake mpya- hususan ikizingatiwa wiki ijayo, Yanga itacheza na wapinzani wao wa jadi, Simba SC katika mechi ya Nani Mtani Jembe 2.
  Na ilikuwa fursa nzuri pia kwa wana Yanga kumuona mchezaji wao huyo mpya kwa mara ya kwanza, ili waujue uwezo wake.
  Lakini bahati mbaya sana haikuwa hivyo- sijui waliondoka uwanjani wanasema nini. Sijui wanamfikiriaje sasa kocha wao, Mbrazil Marcio Maximo. Sijui.
  Nasema sijui kwa sababu, historia ya Emerson kutua Yanga SC inaanzia kwa mchezaji mwingine Mbrazil, Genilson Santana Santos ‘Jaja’.
  Mwanzoni mwa msimu Yanga SC ilisajili wachezaji wawili wa Kibrazil, kiungo Andrey Coutinho na mshambuliaji Jaja, ambao walifanya idadi ya Wabrazil wafanyao kazi Jangwani kufika wanne, baada ya makocha Maximo na Msaidizi wake, Leonardo Leiva.
  Baada ya mechi saba za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Jaja akifunga bao moja tu, alipokwenda kwao kwa mapumziko, hakurejea Tanzania.
  Maximo alisema Jaja amesema ana matatizo ya kifamilia hatarejea na badala yake anamleta Emerson, kiungo mkabaji, aliyemsifia anamjua uwezo wake, ni mzuri.
  Kuacha mshambuliaji hadi kusajili kiungo, tena wa ulinzi- hapa sikumuelewa Maximo na matokeo yake sasa klabu inahaha kusaka mshambuliaji mwingine.
  Hata sakata la kuondoka kwa Emmanuel Okwi linaanzia kwa Maximo mwenyewe, ambaye alimkataa Mganda huyo ili abaki na Jaja.
  Tuchukulie kama yote yamepita, ya Okwi na Jaja na sasa tutazame ukurasa mpya wa Emerson. Jana amepandishwa jukwaani. Kwa nini?
  Inakuwaje mchezaji mpya aanzie jukwaani. Sijui! Hakuwa majeruhi hilo hata baadhi ya wachezaji wa Yanga SC niliozungumza nao jana walinihakikishia.
  Mashabiki wa Yanga SC walimpokea kwa heshima kubwa Maximo Julai mwaka huu wakati anakuja na wameendelea kumuheshimu hadi jana.
  Lakini kama bado wanakumbuka ya Jaja, na tena wanaona mchezaji mpya Emerson anakuja kutoka Brazil na kukaa jukwaani, hiyo heshima italindwa na kipi!
  Bado sijui kama Yanga SC wanavutiwa na kiwango cha timu yao tangu Maximo aanze kazi- najua wanavutiwa na uwezo wa wachezaji wao mmoja mmoja.
  Yanga SC ina mafundi wengi. Hilo nina uhakika nalo. Ila sina uhakika kama kiwango cha uchezaji cha timu kwa ujumla kama kinavutia.
  Na sijui kwa ujumla hivi sasa Yanga SC wanamchukuliaje Maximo. Alamsiki. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIJUI YANGA SC WANAMCHUKULIAJE MAXIMO KWA SASA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top