• HABARI MPYA

  Wednesday, December 10, 2014

  SHERMAN ATUA YANGA SC NA KUSEMA; “NIMEFURAHI SANA, NIKO TAYARI KWA KAZI”

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Liberia, Kpah Sean Sherman amewasili jioni ya leo mjini Dar es Salaam tayari kujiunga na klabu ya Yanga SC.
  Mara baada ya kuwasili, Sherman alisema; “Nina furaha sana kufika hapa salama, natarajia kila kitu kitakwenda vizuri na nitakuwa mchezaji wa Yanga. Nipo tayari kukabiliana na changamoto mpya,”amesema. 
  Awali, Sherman ilikuwa afike jana Dar es Salaam, lakini akakosa ndege ya kuunganisha mapema mjini Istanbul, Uturuki akitokea Cyprus na leo amefika Saa 9:00 Alasiri, Dar es Salaam.
  BIN ZUBEIRY inafahamu Kpah anatarajiwa kufikia vipimo vya afya ambavyo akifuzu atapewa Mkataba wa mwaka mmoja, baada ya mazungumzo ya awali na uongozi wa klabu hiyo.
  Sherman mwenye umri wa miaka 22 anakuja Yanga SC akitokea klabu ya Cetinkaya ya Ligi Kuu ya Cyprus Kaskazini, ambako analazimika kuvunja Mkataba wake uliobakiza miezi minne.
  Kpah Sherman kulia akiwa na Meneja wa Yanga SC, Hafidh Saleh baada ya kuwasili Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam (JNIA) jioni ya leo
  Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Liberia akiwa kwenye gari kwa safari ya hotelini

  Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali kwenye mitandao, Sherman anaonekana ni mshambuliaji hatari na kijana mdogo, ambaye kama Yanga SC wakifanikiwa kumpata na akabahatika kung’ara katika soka ya Tanzania, watakuwa wamelamba ‘dume’.
  Alianza kuichezea Cetinkaya mwaka 2012, akitokea Duzkaya SK aliyoanza kuichezea mwaka 
  2010, akitokea Barrack YC ya nyumbani kwao, Liberia ambayo alianza kuichezea mwaka 2009.
  Sherman akifanikiwa kusaini Yanga SC, atakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa dirisha la dogo baada ya kiungo mkabaji Mbrazil, Emerson de Oliviera Roque na mshambuliaji mzalendo, Danny Mrwanda aliyekuwa anacheza Vietnam.
  Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu Yanga SC kama itamsajili Sherman mkali wa mabao katika Ligi ya Cyprus Kaskazini, italazimika kukata mchezaji mmoja wa kigeni ili ikidhi kanuni ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inayotaka wageni watano tu.
  Bila ya Sherman, tayari Yanga SC inao Wabrazil Emerson, Andrey Coutinho, Wanyarwanda Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite na Mganda Hamisi Kiiza.  
  Na kama Sherman atafanikiwa kusajiliwa Yanga SC atakuwa Mliberia wa pili kucheza Tanzania, baada ya William Fahnbullar aliyewika Simba SC kuanzia 1997 hadi 1999 alipohamia Kajumulo WS kabla ya kutimkia Ulaya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SHERMAN ATUA YANGA SC NA KUSEMA; “NIMEFURAHI SANA, NIKO TAYARI KWA KAZI” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top