• HABARI MPYA

  Tuesday, December 16, 2014

  OKWI ALAMBA MAMILIONI ASAINI MKATABA MNONO SIMBA SC

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI Mganda, Emmanuel Arnold Okwi leo amesaini Mkataba mpya na Simba wa miaka miwili, huku ule wa awali wa miezi sita ukielekea ukingoni.
  Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, wameamua kumuongezea Mkataba Okwi baada ya kuvutiwa na huduma zake.
  Okwi amerejea Simba SC Agosti mwaka huu, baada ya kutemwa na Yanga SC iliyomsajili kutoka Etoile du Sahel ya Tunisia.
  Okwi alijiunga na Etoile kwa dau la dola 300,000 za Kimarekani zaidi ya Sh. Milioni 500 akitokea Simba SC Januari mwaka jana, lakini kufika Mei akatibuana na klabu hiyo.
  Emmanuel Okwi kulia akisaini Mkataba wa kuendelea kuichezea Simba SC, huku akishuhudiwa na Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva

  Klabu ilidai Okwi alipewa ruhusa ya kwenda kuchezea timu yake ya taifa, The Cranes akachelewa kurudi zaidi ya mwezi mzima, wakati mchezaji akadai alikuwa halipiwi mishahara.
  Okwi na Etoile wakafunguliana kesi Shirikisho la Soka la Kimataia (FIFA) na mchezaji huyo wa Uganda akaomba aruhusiwe kuchezea timu nyingine kunusuru kipaji chake wakati sakata hilo linaendelea.
  FIFA ikatoa ruhusa hiyo na Okwi akajiunga na klabu yake ya zamani, SC Villa ya Uganda lakini baada ya miezi sita, akasajiliwa na Yanga SC kwa Mkataba wa miaka miwili na nusu Desemba mwaka jana.
  Hata hivyo, kufika Machi mwaka huu, Okwi akatibuana na Yanga SC na kuamua kuomba kurejea klabu yake, Simba SC ambako alifanikiwa. Yanga SC walifungua kesi TFF kupinga, lakini mshambuliaji huyo wa Uganda akawagaragaza na kupewa ridhaa ya kuendelea na kazi Simba SC, ambako alipewa Mkataba wa miezi sita.
  Na baada ya kuionzoza timu hiyo kama Nahodha kushinda mbili 2-0 dhidi ya mahasimu Yanga SC, katika mchezo wa Nani Mtani Jembe Jumamosi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Okwi leo amepewa Mkataba mpya ambao umemfanya avune mamilioni kibao, siri yao Simba na yeye mwenywe. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: OKWI ALAMBA MAMILIONI ASAINI MKATABA MNONO SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top