• HABARI MPYA

  Monday, December 15, 2014

  MSANII WA DANSI ANAYEKATAA KUHAMA KWA MILIONI 15 NAYE AKAPIMWE AKILI

  Wiki iliyopita niliandika kuwa mmiliki wa bendi anayetaka kumchukua msanii wa muziki wa dansi kwa milioni 15 akapimwe akili, lakini leo nageukia upande wa pili, nasema msanii wa dansi anayekataa kuhama kwa milioni 15 naye anastahili kupimwa akili.
  Wakati mwingine kwenye muziki, hususan muziki wa haya mabendi yetu kuna raha zake, hakuna msongo wa mawazo kama kwenye soka.
  Kwenye soka mchezaji ghali anaponunuliwa na timu fulani, hupimwa kwa matokeo mazuri anayochangia, kama ni mshambuliaji basi ajue kucheka na nyavu, kama ni beki ajue kudhibiti timu isifungwe, kama ni kipa basi awe mkali wa kuokoa michomo ya hatari inayoelekezwa langoni mwake.

  Kama ni kocha ndo usiseme, timu likivurunda tu, mashabiki hawakawii kukuambia “TUACHIE TIMU YETU”, wamiliki nao kuvunja mkataba wako ni kama kufumba na kufumbua, hakuna ushindi, hakuna udugu.
  Lakini kwenye muziki, hakuna hilo, hakuna kipimo cha maana atakachopimwa nacho msanii – mashabiki waongezeke au wasiongezeke hilo wala halimuhusu, ndo maana nasema kwenye muziki kuna raha yake kwa msanii.
  Kutokana na ugumu wa biashara ya muziki wa dansi, maisha ya baadhi ya wasanii wake yamekuwa hayatabiriki, yako kama homa ya vipindi, leo mazuri mara kesho mabaya.
  Bendi nyingi zimepoteza uwezo wa kulipa mishahara ya wasanii kwa muda unaostahili, zimepoteza uwezo wa kuwatibia wasanii wake, zimepoteza uwezo wa kuwalipia pango, ni kipindi cha mpito ambacho hakikwepeki.
  Ni wakati ambao kila msanii anapaswa kuitumia vizuri nafasi adimu anayoipata ya kutengeneza pesa, ni nafasi ambayo inaweza kuja mara moja tu katika maisha yao, ukiipoteza hairudi tena.
  Na ni hapo ndipo ninaposema msanii anayekataa kuhama bendi kwa milioni 15 au hata 10 au hata 8, basi anastahili kupimwa akili.
  Upo katika bendi X unalipwa labda shilingi laki mbili kwa mwezi tena bila mkataba, kisha inakuja bendi Y inakutongoza ikupe mkataba wa mwaka mmoja, wanakuahidi kukupa kila unachopewa na bendi X, lakini juu ya yote wanakuambia kuna bakshishi ya milioni 15 au 10 au 8 kama donge nono la kukushawishi kujiunga nao. Unakataa.
  Unakataa kwa kuwa una mapenzi makubwa na bendi unayoitumikia, unakataa kwa kuwa wenye bendi wamekutoa mbali sana, unakataa kwa kuambiwa vuta subira mambo yakiwa mazuri utawezeshwa mshiko unaofanana na huo.
  Uzoefu unaonyesha wazi kuwa milango huwa iko wazi siku zote, unaweza ukaondoka leo na kisha mwaka ujao ukapokelewa ukitaka kurudi, tena pengine na pesa nono juu yake.
  Ni ujinga kukataa pesa kama hizo kwa kipindi hiki kigumu cha maisha ya muziki wa dansi, uamuzi sahihi ni kuchukua mshiko, unaondoka bila kunyea kambi ili baada ya mwaka mmoja urejee kwa amani kwenye bendi ambayo eti una mapenzi nayo ya dhati.
  Ipo mifano mingi ya wasanii waliokataa mamilioni ya pesa, lakini hadi leo hii hawajapewa hata robo ya kile walichokua wakipate kwenye bendi mpya, kwa sasa hawatakiwi tena hata kwa milioni moja. Wanajuta.
  Muziki ni ofisi kama ofisi kama ofisi zingine, muziki ni maisha, msiishi kwa mazoea, unakataaje pesa za bure tena zilizoko kwenye maandishi ya kisheria, mkataba mfupi wa mwaka mmoja au miliwili baada ya hapo unaangalia upepo mwingine. Ni kwanini usistahili kupimwa akili?
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MSANII WA DANSI ANAYEKATAA KUHAMA KWA MILIONI 15 NAYE AKAPIMWE AKILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top