• HABARI MPYA

  Wednesday, December 03, 2014

  MASHINDANO YA BASEBALL TAIFA KUFANYIKA AZANIA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU tano zinashiriki katika mashindano ya Kitaifa ya Mchezo wa baseball yajulikanayo kama ‘Sport for Tomorrow’ yatakayofanyika mwishoni mwa juma katika Shule ya Azania ili kupata timu ya Taifa itakayoshiriki katika mashindao ya kimataifa yatakayofayika nchini Kenya baadaye mwezi huu.
  Timu hizi ambazo ni Kilimanjaro ikiwakilishwa na Shule ya Sekondari ya Sanya Juu, Ruvuma itawakilishwa na Shule ya Sekondari ya Londoni, Mwanza itawakilishwa na Shule ya Sekondari St Marys, Temeke itawakilishwa na Shule ya Sekondari ya Kibasila, Ilala itawakilishwa na Shule ya Sekondari ya Azania na Zanzibar itawakilishwa na Shule ya Sekondari ya Mwanakerekwe C.
  Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Chama cha Mchezo wa Baseball Tanzania (TaBSA) ambao ndio waandaaji wa mashindano hayo, Ahmed Makata, alisema mashindano haya yatatumika kuchagua wachezaji wa Timu ya Taifa itakayoshiriki katika mashindano ya KImataifa ya wachezaji wa umri chini ya miaka 17 yatakayofanyika nchini Kenya  Kuanzia Disemba 15 hadi 20 mwaka huu.

  Kocha wa Timu ya Taifa ya Mchezo wa baseball Shinya Tomanari akielezea jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kutangaza mashindano ya KItaifa ya mchezo huo yatakayofanyika katika shule ya Azania JUmamosi na Jumapili. Katikati ni Balozi mdogo wa Japan nchini, Kazuyashi Matsunaga na Katibu Mkuu wa Chama cha Baseball Tanzania (TABSA), Alpherio Nchimbi.

  Aliwatalka watanzania wauchukulie mchezo huo kwa uzito unaostahili kwani ni mchezo unaolipa na wachezaji wake ni miongoni mwa watu wanaolipwa fedha nyingi katika michezo duniani.
  “Wengi wanadhani mchezo huu ni kwa nchi maarufu tu kama  Marekani na Japan lakini ukweli ni kuwa mchezo huu umeanza kujizolea umaarufu sana hasa katika nchi za Afrika,” alisema.
  Naye Katibu Mkuu wa TaBSA , Alpherio Nchimbi alisema wachezaji wote wamekuwa wakijiandaa vizuri mwaka mzima kwa mashindano haya na inatia moyo. 
  “Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha mchezo huu unakuwa maarufu nchini kwani ni jukwaa zuri la kuunganisha vijana na kuwafanya wawe na ushirikiano,” alisema.
  Balozi mdogo wa Japan nchini, Kazuyashi Matsunaga alisema Programu hii ya Sport for Tomorrow ilianzishwa na Serikali ya Japan na ina lengo la kusambaza michezo kwa watu zaidi ya milioni 10 katika nchi zaidi ya 100 hadi mwaka 2020 ambapo mashindano ya Olympics na Paralympic yatafanyika nchini humo.
  Alisema nchi yake imechangia Dola za Kimarekani 9000 kwa ajili ya mashindano ya Dar es Salaam katika Shule ya Azania.
  Alisema mashindano haya ndio ya kwanza katika mashindano yanayotokea katika program hii duniani na kuongeza kuwa anaamini mchezo huu utasaidia kuleta maendeleo nchini Tanzania.
  Katika mkutano wa jana pia ilifanyika draw ya kupanga timu zitakazocheza JUmamosi na Jumapili. Kundi A itajumuisha KIbasila, Sanya Juu na Londoni wakati Kundi B itajumuisha Azania na St Marys.
  Hata hivyo timu ya Londoni haitacheza hatua ya awali hivyo basi mshindi kati ya Kibasila na Sanya Juu atacheza na Londoni. Shule hii ilipewa upendeleo wa aina yake kwa kuwa imetoka mbali na ni mojawapo ya njia ya kuwahamasisha wachezaji wake.
  Mashindano haya, ambayo yanatarajiwa kufunguliwa na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, JUma Mkamia, hayatakuwa na kiingilio na yataanza saa moja na nusu asubuhi hadi saa kumi na nusu jioni Jumamosi na Jumapili.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MASHINDANO YA BASEBALL TAIFA KUFANYIKA AZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top