• HABARI MPYA

  Monday, December 08, 2014

  HANS POPPE APAGAWA NA 4-2 ZA MTIBWA JANA AKIIFIKIRIA YANGA JUMAMOSI MTANI JEMBE

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  KIPIGO cha mabao 4-2 kutoka kwa Mtibwa Sugar jana kimeonekana kabisa kumchanganya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe hasa akizingatia anaelekea kwenye mechi na mahasimu Yanga SC Jumamosi.
  Simba itamenyana na Yanga SC Jumamosi katika mchezo wa Nani Mtani Jembe 2, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikitoka kwenye kipigo cha 4-2 jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar.
  Hans Poppe aliyekuwa ameketi jukwaa kuu katika Uwanja ‘simpo’ na wa kisasa unaomilikiwa na Azam FC pamoja na Makamu wa Rais wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ hakuwa na raha hata kidogo na alionekana kutawaliwa na maswali mengi kuliko majibu.
  Hans Poppe kulia akizungumza na Kaburu wakati wa mchezo wa jana Chamazi
  Hans Poppe akiwa ameshika tama jana Azam Complex

  Hans Poppe akitoa dukuduku lake kwa kocha Matola

  Alikuwa akizungumza na Kaburu kwa ishara za kukerwa, kukasirika na kukata tamaa na baada ya mchezo akateremka kuwafuata makocha.
  Hakupata fursa ya kuzungumza na kocha Mkuu, Patrick Phiri raia wa Zambia kwa sababu wakati huo alikuwa akizungumza na Waandishi wa Habari, lakini akamkamata kocha Msaidizi, Suleiman Matola.
  Walizungumza na Matola kwa dakika kadhaa kisha wakaachana na timu hiyo ikaondoka.
  Kipa namba moja, Ivo Mapunda ndiye aliyekuwa langoni jana wakati Simba SC ikibugizwa mabao manne, lakini udhaifu kwa ujumla ulionekana kwenye safu ya ulinzi.
  Kukosekana kwa sentahafu na Nahodha Mganda, Joseph Owino na kiungo mkabaji, Jonas Mkude dhahiri kulionekana kuifanya Simba ipwaye jana na mambo yalikuwa mabaya zaidi baada ya kiungo Said Ndemla kuumia dakika ya 45 na kumpisha Mrundi Pierre Kwizera.  
  Simba SC ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao jana, mfungaji Ndemla kabla ya Mussa Hassan Mgosi kuisawazishia Mtibwa Sugar dakika ya 28.
  Kipindi cha pili, Mtibwa inayofundishwa na Nahodha wake wa zamani, Mecky Mexime ilifanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 51, ingawa alionekana kama aliupiga mpira mkononi mwa kipa Ivo Mapunda.
  Mohammed Ibrahim aliyeingia kuchukua nafasi ya Mgosi kipindi cha pili, aliifungia Mtibwa Sugar bao la tatu dakika ya 73, akiunganisha krosi ya Nahodha wa zamani wa Simba SC, Henry Joseph Shindika.
  Ame Ally aliyeingia kuchukua nafasi ya Abdallah Juma aliifungia Mtibwa Sugar bao la nne dakika ya 58, kabla ya Simba SC kupata bao la pili lililofungwa na Amisi Tambwe dakika ya 89 kwa penalti, kufuatia David Luhende kumsukuma Shaaban Kisiga ‘Malone’ kwenye eneo la hatari.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HANS POPPE APAGAWA NA 4-2 ZA MTIBWA JANA AKIIFIKIRIA YANGA JUMAMOSI MTANI JEMBE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top