• HABARI MPYA

  Monday, December 15, 2014

  CECAFA KUBADILISHA MUUNDO WA MICHUANO YAKE, CHALLENGE 2014 YAZIKWA RASMI NAIROBI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limeamua rasmi kuachana na ndoto za kufanya Kombe la Challenge mwaka huu, na badala yake kuelekeza nguvu katika mashindano ya mwakani.
  Taarifa ya Katibu wa CECAFA kwa BIN ZUBEIRY, imesema kwamba hayo yamefikiwa katika Mkutano Mkuu wa dharula wa bodi hiyo uliofanyika jana mjini Nairobi, Kenya chini ya Mwenyekiti wake, Mhandisi Leodegar Chillah Tenga.
  Mkutano huo, ulihudhuriwa na viongozi wakuu 11 kati ya 12 wa Vyama na Mashirikisho ya Soka Afrika Mashariki na Kati, Jamal Malinzi (Tanzania), Sam Nyamweya (Kenya), Moses Magogo (Uganda), Vincent Nzamwita (Rwanda), Goc Chabur (Sudan Kusini), Reverien Ndikuriyo (Burundi), Abdiqaani Saed (Somalia), Tesfaye Gebreyesus (Eritrea), Juneidi Basha (Ethiopia) Ahmed Eltrifi (Sudan) na Ravia Idarius (Zanzibar).
  Mwenyekiti wa CECAFA, Leodegar Tenga (katikati) na Katibu wake, Nico Musonye kushoto

  Baada ya saa nne za michango na mijadala, CECAFA imefikia uamuzi wa kubadilisha muundo wa mashindano yake ili kupunguza gharama na kuongeza mvuto wake. 
  Pamoja na hayo, CECAFA wamekubaliana kuendelea kumuunga mkono, Rais wa sasa CAF, Issa Hayatou na rais wa FIFA, Sepp Blatter katika uchaguzi wa mwakani. 
  Michuano ya Challenge ilipangwa kufanyika Ethiopia mwaka huu, lakini wenyeji hao wakajitoa dakika za mwishoni na jitihada za CECAFA kupata nchi mbadala wa kuandaa mashindano hayo hazikufanikiwa.
  Tayari Rwanda imepewa uenyeji wa Challenge ya mwakani, kama sehemu ya kujipima kabla ya kuipokea michuano ya CHAN. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: CECAFA KUBADILISHA MUUNDO WA MICHUANO YAKE, CHALLENGE 2014 YAZIKWA RASMI NAIROBI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top