• HABARI MPYA

  Tuesday, December 09, 2014

  BURUNDI WALITIA MCHANGA PILAU LA UHURU, WAICHAPA 2-1 STARS MABORESHO TAIFA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KIKOSI cha pili cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, maarufu kama ‘Taifa Stars Maboresho’ jioni hii kimefungwa mabao 2-1 na Burundi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Katika mechi hiyo maalum iliyoandaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kusherehekea miaka 53 ya Uhuru, Stars Maboresho ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 11 kupitia kwa Yussuf Rashid.
  Burundi walichangamka baada ya bao hilo na kuanza kusukuma mashambulizi ya nguvu langoni mwa Maboresho iliyoongozwa na Kocha Mkuu wa Tanzania, Mholanzi Mart Nooij.
  Mshambuliaji wa Tanzania, Atupele Green akiwa amekaa chini huku Abbas Nshimirimana wa Burundi akiufuata mpira

  Kwa kutumia vyema udhaifu wa safu ya kiungo ya Tanzania, Burundi walitawala mchezo na kufanikiwa na kupata bao la kusawazisha dakika ya 25, mfungaji Fabrice Mimimahazwe kabla ya kupata bao la ushindi dakika ya 72 kupitia kwa Nassor Niyonkuru.
  Maboresho walicharuka baada ya kufungwa bao la pili na kuanza kushambulia mfululizo, lakini kipa wa Burundi, Innocent Mbonihankuye alikuwa kikwazo kwao kupata bao.
  Kwa ujumla, Stars Maboresho haikucheza soka ya kuvutia na maana yake Mart Nooij ana kazi kubwa ya kufanya kuiboresha timu hiyo.  
  Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Aishi Manula, Miraj Adam, Gardiel Michael, Joram Mgeveke/Emmanuel Semwanda dk90, Vencent Andrew, Salum Mbonde, Rashid Yussuf/Omar Njenje dk80, Hassan Banda, Atupele Green, Kelvin Friday/Mohammed Abubakar dk70 na Hussein Moshi/Ramadhani Shiza dk62.
  Burundi; Innocent Mbonihankuye, Issa Hakizimana, Rashid Nshimirimana/Rashid Hererimana dk56, Nassor Niyonkuru/Shassih Nahimana dk73, Fataki Kiza, Emmanuel Nyuyekure, Christopher Nduwarugira/Omar Ngando dk89, Abbas Nshimirimana, Fabrice Mimimahazwe/Tressor Akimana dk64, Laudit Mayugo/Tressor Mubango dk76,  Abdul Razak Fiston na Amisi Kandolo.
  Kevin Friday wa Tanzania kulia akitafuta mboni za kumtoka beki wa Burundi, Nassor Niyonkuru
  Beki wa Tanzania, Miraj Adam akimtoka beki wa Burundi, Fataki Kiza
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BURUNDI WALITIA MCHANGA PILAU LA UHURU, WAICHAPA 2-1 STARS MABORESHO TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top