• HABARI MPYA

  Wednesday, December 10, 2014

  AZAM FC WAENDA UGANDA KESHO KUWEKA KAMBI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  AZAM FC  wanaondoka kesho Dar es Salaam kwenda Kampala, Uganda kuweka kambi ya siku 10 kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba amesema kwamba ziara hiyo ni maalum kwa timu kujiandaa na Ligi Kuu na kikosi kitarejea Desemba 22, mwaka huu.
  Ligi Kuu iliyosimama kwa muda Novemba 9, baada ya mechi saba, inatarajiwa kuanza tena Desemba 26, mwaka huu.
  Azam FC imefanya usajili wa wachezaji wawili tu katika dirisha dogo, ambao beki wa kati Serge Wawa Pascal, raia wa Ivory Coast aliyekuwa anacheza El Merreikh ya Sudan na kiungo Amri Kiemba aliyesajiliwa kwa mkopo kutoka Simba SC.
  Kikosi cha Azam FC ambacho kinakwenda Kampala kesho
   

  Pamoja na hayo, mabingwa hao wa Tanzania Bara wamemchukua kocha Mganda, George ‘Best’ Nsimbe kuziba pengo la Muingereza, Kali Ongala aliyejiuzulu baada ya mechi sita.
  Azam FC imeonyesha iko vizuri chini ya benchi jipya la ufundi, linaloongozwa na kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog baada ya jana kuwafunga vinara wa Ligi Kuu, Mtibwa Sugar mabao 3-1. 
  Katika mchezo huo maalum uliondaliwa kujaribu taa za Uwanja wa Azam Complex, hadi mapumziko tayari Azam FC walikuwa mbele kwa mabao hayo 3-1, yaliyofungwa Didier Kavumbangu dakika ya nne, Aggrey Morris dakika ya 15 na Khamis Mcha ‘Vialli’ dakika ya 45.
  Kavumbangu alifunga akimalizia mpira uliookolewa na kipa kufuatia shuti dhaifu la Kipre Tchetche, wakati Morris alifunga kwa mpira wa adhabu umbali wa mita 20 na Mcha alifunga ndani ya boksi kufuatia kona ya Mudathir Yahya.
  Bao la Mtibwa lilifungwa na mkongwe Mussa Hassan Mgosi kwa penalti dakika ya 35 kufuatia beki Serge Wawa Pascal kuunawa mpira kwenye boksi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC WAENDA UGANDA KESHO KUWEKA KAMBI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top