• HABARI MPYA

    Saturday, March 24, 2012

    MJUE NSA JOB MAHENYA, STRIKER ALIYEKIPIGA UJERUMANI

    
    Nsa Job akibunika tik tak mbele ya Juma Nyosso na Mohamed Banka Yanga ilipocheza na Simba mwaka juzi
    
    Nswa Job kulia akimtoka Mzungu enzi hizo akiwa Yanga
    DORIS MALIYAGA
    WAPO wachezaji ambao hupata mafanikio baada ya kusota kwa muda mrefu na Nsa Job Mahenya ni mmoja wao.
    Nsa, ambaye ni mshambuliaji wa Villa Squad, amethibitisha hilo baada ya kufanya vizuri katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
    Amefunga mabao nane katika mechi sita, hali iliyomvutia Kocha Mkuu wa Taifa Stars Jan Paulsen, amwite katika kikosi chake kwa mara ya kwanza.
    Hiyo ni bahati na rekodi kwake, kwani katika msimu uliopita akiwa na Yanga, Nsa alipita katika kipindi kigumu na mwenyewe amekiri hatasahau.
    Akiwa na kikosi hicho cha Jangwani, alicheza mechi zote za mzunguko wa kwanza msimu uliopita bila kufunga bao, hali iliyosababisha kupachikwa jina la Kazi Bure.
    Jina la `Kazi Bure' lilitokana na kuwa machachari kutengeneza nafasi lakini alikuwa anashindwa kufunga.
    Sasa imekuwa kinyume, kwa sababu Nsa wa leo anaonekana lulu yenye thamani kwa mashabiki kutokana na alivyoibuka katika kufunga mabao na kuzivutia klabu mbalimbali zikitamani ziwe naye kikosini.
    Mwanaspoti ilifanya naye mahojiano ili aeleze siri ya mafanikio yake.

    Kutoka Kazi Bure hadi Taifa Stars
    Nsa, ambaye anakiamini kipaji chake anasema: ''Nina uwezo wa kufanya vizuri katika timu yoyote. Siri kubwa ya mafanikio yangu kama nilivyosema, nilijitambua na kuongeza bidii kuhakikisha nafanikiwa kwa kile nilichokikusudia.
    Nimepita katika kipindi kigumu nikiwa na Yanga na chote nilikubaliana nacho kwa sababu nilijitambua," anasema Nsa anayependa soka la kiungo wa Liverpool, Steven Gerard.
    Mashabiki watambue kuwa, vipindi kama hivi huwa vinatokea kwa kila mchezaji, inaweza kuwa mbaya na wakati mwingine furaha kwa sababu tutafanya vizuri.
    "Yanga niliingia kwa mafanikio na kama ulivyoona nilipata namba na kucheza mechi zote za mzunguko wa kwanza pamoja na kuwa sikufunga bao, kocha (Kostadin Papic) aliniamini na kuendelea kunipa nafasi kwa sababu alifahamu umuhimu wangu hapo," alisisitiza Nsa, ambaye mabao yake nane sasa yamemuweka katika kinyang'anyiro cha ufungaji bora.
    Nsa anakwenda mbali na kueleza kwa kutolea mfano mshambuliaji wa Chelsea, Fernando Tores, ambaye wakati yupo Liverpool alikuwa akifunga mabao mengi na tegemeo kikosini hapo, lakini alipohamia Chelsea hali ikawa ngumu kwake akashindwa kufanya vizuri.
    Uwezo wake wa sasa, anasema, umemfanya adhihirishe kwamba anaweza kubadilika na ndiyo maana ametoka kwenye jina la 'Kazi Bure' na kuingia katika orodha ya wachezaji mahiri kiasi cha kuitwa Taifa Stars.
    Amesisitiza: "Mashabiki watambue kuwa, Nsa amepita kipindi kigumu, ni mambo ya mpira.
     "Nsa ni yule yule, anajitambua na hajabadilika, isipokuwa sasa ni wakati wangu, hakuna sababu yoyote inayochangia kuhusu mabadiliko yangu," anaeleza Nsa, anayeishabikia pia klabu ya Liverpool ya England.
    Kuhusu nafasi na mfumo wa Villa, Nsa anaeleza: "Hakuna tofauti yoyote kati ya Yanga na Villa, na kama ninavyosema, yale yalikuwa matatizo ya mpira tu na si mambo mengine.
    "Mchezaji hana sababu ya kuchagua watu wa kucheza nao japo mara nyingine inasaidia, lakini kwa upande wangu si sababu, kwani hata hao niliokuwa nikicheza nao Yanga tulikuwa pamoja kwa muda mrefu, tukazoweana."

    Kilichomng'oa Yanga
    "Kuondoka kwangu Yanga hakukuchangiwa na kushuka kwa kiwango, niliondoka pale kutokana na mambo tofauti," anaeleza Nsa.
    "Kulikuwa na matatizo mengine, si unajua mambo ya timu kubwa hizi."

    Yanga, Simba na Azam FC
    Nsa alizichezea klabu tatu zinazofanya vizuri katika Ligi Kuu Bara kwa vipindi tofauti kama Simba, Yanga na Azam FC hadi kutua Villa.
    "Maisha ya klabu hizo nayajua kwa sababu zote nimecheza, hakuna anayenidanganya, kila moja ina faida na matatizo yake."
    Ameeleza kuwa, yuko tayari kujiunga na klabu yoyote kati ya hizo au nyingine katika ligi kwa sababu mpira ndiyo ajira yake.
    "Naweza kuichezea klabu yoyote itakayo nihitaji kwa sasa, najiamini na naamini kwa kiwango changau cha sasa, nitaifanyia mazuri na kutimiza malengo katika Villa," alisisitiza Nsa, ambaye mkataba wake na Villa unamalizika mwisho wa msimu huu.

    Taifa Stars
    "Kuitwa Taifa Stars, ilikuwa ni sehemu ya ndoto zangu, nimefurahi baada ya kutimia kwani kila mchezaji anatamani kuchezea Taifa Stars," anaeleza.
    ''Nafasi hii nitaitumia kama changamoto ya kufanya vizuri na kukamilisha malengo ya maisha yangu ya soka, naamini kwa uwezo wa Mungu nitafanikiwa."

    Historia
    Nsa ni mtoto wa Diwani wa Kata ya Misufini, Morogoro, Mzee Job. Ni mtoto wa nne kuzaliwa katika familia yao yenye watoto watano.
    Ndugu zake ni pamoja na dada yake wa kwanza, Anna, Geoffrey, Ruth na mdogo wake Sinayi.
    Alisoma katika Shule ya Msingi ya Nguzo na baadaye Shule ya Sekondari ya Forest Hill, zote za Morogoro kabla ya kuhamia Makongo ambako ndiko alimaliza kidato cha nne.
    Anasema alihamia Makongo baada ya Mkuu wa shule hiyo, Kanali Idd Kipingu, kugundua kipaji chake, baada ya kumaliza ndipo akasajiliwa na Moro United ilipokuwa chini ya Merei Balhabou.
    Hata hivyo, kabla ya kufika hapo, alipata umaarufu akiwa na timu yake ya Juventus ya mtaa wa Misufini, Morogoro.
    Pia aliwahi kufanya majaribio nchini Ujerumani katika klabu ya Borussia Dortmund kwa kipindi cha miezi sita mara baada ya kuondoka Moro United mwaka 2006, lakini hakufanikiwa kuchaguliwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MJUE NSA JOB MAHENYA, STRIKER ALIYEKIPIGA UJERUMANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top