• HABARI MPYA

    Friday, November 16, 2018

    SHOMARI KAPOMBE AUMIA MAZOEZINI NA ATAKOSEKANA TAIFA STARS IKIVAA LESOTHO JUMAPILI MASERU KUFUZU AFCON

    Na Saada Salmin, DAR ES SALAAM
    BEKI wa kulia wa Tanzania, Shomari Kapombe ataukosa mchezo wa Jumapili dhidi ya Lesotho Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon dhidi ya wenyeji Lesotho kutokana na kuwa majeruhi.
    Taifa Stars watakuwa wageni wa Mamba wa Lesotho Jumapili Uwanja wa Setsoto mjini Maseru kuanzia Saa 11:00 jioni na Kapombe anayeweza kucheza kama kiungo pia hataweza kucheza kutokana na maumivu ya enka.
    Meneja wa Taifa Stars, Danny Msangi ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwa simu kuoka Maseru kwamba Kapombe aliumia juzi katika mazoezi ya jioni kwenye kambi ya Bloemfontein, Afrika Kusini.
    Msangi amesema kwamba Kapombe aliukanyaga mpira vibaya, mguu ukacheza na kusababisha maumivu ya kifundo cha mguu na pamoja na jitihada za madakatri wa timu, Richard Yomba na Gilbert Kigadya kumtibu, lakini hajapata nafuu na imethibitishwa hatacheza keshokutwa.
    Shomari Kapombe ataukosa mchezo wa Jumapili dhidi ya Lesotho Kundi L kufuzu AFCON ya mwakani nchini Cameroon

    Kapombe, beki wa kulia wa Simba SC ya Dar es Salaam aliyewahi kuchezea AS Cannes ya Ufaransa,  anakuwa mchezaji wa pili kuthibitika hatacheza Jumapili, baada ya mshambuliaji wa BDF XI ya Botswana, Rashid Mandawa.
    Kuumia kwa Kapombe, mchezaji wa zamani wa Azam FC ni pigo kwa timu kutokana na kuwa mchezaji mwenye maarifa mengi mbali na uwezo wake na kiongozi pia wa wachezaji wenzake uwanjani, ingawa nafasi yake itazibwa na Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia.
    Maana yake, Taifa Stars itawakosa wachezaji wawili kutoka kikosi kilichoifunga Cape Verde 2-0 Oktoba 16 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, mwingine ni Nahodha, Mbwana Samatta ambaye anatumikia adhabu ya kadi za njano.
    Kikosi cha Stars kilichowasili mchana huu Maseru ni; makipa Aishi Manula (Simba SC), Aaron Kalambo (Tanzania Prisons), Beno Kakolanya (Yanga SC) na Benedictor Tinocco wa (Mtibwa Sugar).
    Mabeki ni Hassan Kessy (Nkana FC/Zambia), Abdi Banda (Baroka FC/Afrika Kusini), Shomary Kapombe, Erasto Nyoni (Simba SC), Ally ‘Sonso’ Abdulkarim (Lipuli FC), Kelvin Yondan, Gardiel Michael (Yanga SC), Aggrey Morris na Abdallah Kheri (Azam FC).
    Viungo ni Himid Mao (Petrojet/Misri), Simon Msuva (Difaa Hassan El-Jadidi/Morocco), Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya (Azam FC), Salum Kimenya (Tanzania Prisons), Feisal Salum (Yanga SC), Jonas Mkude na Shiza Kichuya (Simba SC) zote za nyumbani na washambuliaji ni Shaaban Iddi Chilunda (CD Tenerife/Hispania), John Bocco wa Simba SC na Yahya Zayed wa Azam FC zote za nyumbani.
    Kikosi hicho chini ya makocha Emmanuel Amunike anayesaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi na mzawa Hemed Suleiman ‘Morocco’, Meneja Danny Msangi, Mtunza Vifaa Ally Ruvu na Madaktari Richard Yomba na Gilbert Kigadya kitaingia kambini nchini Afrika Kusini wiki ijayo kabla ya kwenda Lesotho siku moja kabla ya mchezo wa Novemba 18.
    Taifa Stars inahitaji ushindi dhidi ya Lesotho Jumapili ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu AFCON ya pili tu kihistoria kwao tangu ile ya mwaka 1980 nchini Nigeria.
    Kwa sasa, Stars inashika nafasi ya pili kwenye Kundi L kwa pointi zake tano baada ya kucheza mechi nne, ikishinda moja, sare moja na kufungwa moja, ikiizidi kwa pointi moja Cape Verde. 
    Uganda ambayo ni kama imekwishafuzu, inaongoza kundi hilo kwa pointi zake 10 za mechi tano pia, wakati Lesotho yenye pointi mbili ni ya mwisho.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SHOMARI KAPOMBE AUMIA MAZOEZINI NA ATAKOSEKANA TAIFA STARS IKIVAA LESOTHO JUMAPILI MASERU KUFUZU AFCON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top