• HABARI MPYA

  Wednesday, November 21, 2018

  KIDAU AIAMBIA MAHAKAMA KWAMBA HAWAJUI ALIYEWALALAMIKIA AKINA MALINZI NA MWESIGWA KUIBA FEDHA ZA TFF

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidau amesema kwamba hawamfahamu aliyewalalamika viongozi wa zamani wa shirikisho hilo, aliyekuwa Rais, Jamal Malinzi na Katibu wake, Selestine Mwesigwa kwamba waliiba fedha za taasisi hiyo.
  Kidau kiungo wa zamani wa Milambo ya Tabora na Simba SC ya Dar es Salaam, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa hadi sasa hafahamu ni nani aliyeiba fedha za shirikisho hilo kwa sababu hawajapata taarifa kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa hesabu.
  Akitoa ushahidi wake katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili aliyekuwa Malinzi na wenzake leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, Kidau amesema kuna upotevu wa fedha ambao umesababisha Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kuwanyima fedha TFF kwa miaka minne mfululizo na kwamba hivi sasa wanahangaika namna ya kuifanya nchi ipate fedha tena.
  Akijibu maswali ya Wakili wa utetezi, Dk Richard Rweyongeza, Kidau aliyefika mahakamani hapo kumalizia ushahidi wake, alidai hafahamu ni nani aliwalalamika akina Malinzi kuiba fedha za TFF na ndiyo maana hadi sasa wapo kimya kwa sababu hawajapata taarifa zozote na ndio maana wapo kimya hawajasema ni nani aliyeiba fedha hizo.
  Aidha, Kidau alidai kuwa aliwahi kupokea fedha kutoka kwa Malinzi wakati timu ya Taifa Stars ilipozuiliwa kutoka hotelini na zikawasaidia kuruhusiwa kuwatoa wachezaji.
  “Baada ya TFF kufungiwa ofisi zake na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), sikuwahi kujua fedha za kuendeshea shirikisho hilo zilitoka wapi kwa sababu sikuwa na shughuli za kila siku na shirikisho kwani nilikuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na tulikuwa tukiitwa baada ya miezi mitatu," alidai Kidau.
  Katibu huyo wa TFF, alidai kuwa kanuni za TFF zinapitishwa na Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo na kwamba katika masuala yoyote ya kubadilisha mtia saini benki ni lazima Rais apeleke ajenda hiyo kwenye kamati na wakikubaliana nayo anaambatanisha pamoja na taarifa za kikao kupeleka benki.
  Awali, akiongozwa na Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, shahidi huyo alidai kuwa kwa mujibu wa kanuni za TFF, taasisi inapohitaji kukopa fedha, inapaswa kuomba ridhaa kwenye Kamati ya Utendaji.
  Alidai kuwa tangu mwaka 2013 hadi 2017 alikuwa mjumbe wa kamati hiyo na kwamba hawajawahi kupata maombi ya kukopa fedha kwenye benki au mtu yoyote kutoka kwa Kamati ya Utendaji.
  "Tangu niingie ofisini kama Mtendaji Mkuu wa shirikisho, sijawahi kupata maombi yoyote wala barua kutoka kwa washitakiwa kwamba wanataka marejesho ya fedha walizotumia," alieleza.
  Aliendelea kudai kuwa Katiba inaelekeza yote yanayopaswa kupitishwa na Kamati ya Utendaji huidhinishwa na Mkutano mkuu wa TFF na ndio utaeleza bajeti ya mwaka ni kiasi gani.
  Kidau alidai kama kuna uhitaji fedha za kukopa ni lazima Kamati ikubaliane na maelezo ikiwa ni pamoja na kuelezwa ni masharti yapi yaliyotolewa na taasisi hizo za mikopo.
  Mbali na Malinzi, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Joas Selestine(46) na Mhasibu wa TFF,  Nsiande Isawayo Mwanga(27).
  Wengine ni Meneja wa  Ofisi TFF, Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya ambao kwa pamoja  wanakabiliwa na mashitaka 30 katika  kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa dola za Marekani 173,335 na Sh 43,100,000.
  Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wanaendelea kusota rumande kwa sababu wanakabiliwa na mashitaka ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KIDAU AIAMBIA MAHAKAMA KWAMBA HAWAJUI ALIYEWALALAMIKIA AKINA MALINZI NA MWESIGWA KUIBA FEDHA ZA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top