• HABARI MPYA

  Ijumaa, Novemba 23, 2018

  REFA AKATAA BAO LA KAGERE DAKIKA ZA LALA SALAMA UWANJA WA TAIFA SIMBA SC YALAZIMISHWA SARE 0-0 NA LIPULI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imelazimishwa sare ya bila kufungana na Lipuli FC ya Iringa katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Kwa sare hiyo, mabingwa hao watetezi wanajiongezea pointi moja na kufikisha 27 baada ya kucheza mechi 12, wakiendelea kushika nafasi ya tatu nyuma ya watani wao wa jadi, Yanga SC wenye pointi 29 za mechi 11 na vinara, Azam FC wenye pointi 33 za mechi 13.
  Kwa Lipuli FC inayofundishwa na Nahodha wa zamani wa Simba SC, Suleiman Abdallah Matola sare ya leo inawafanya wafikishe pointi 13 katika mechi ya 14, wakiwa bado katika eneo la hatari la kushuka daraja, nafasi ya 14 kwenye Ligi Kuu ya timu 20. 

  Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Patrick J Aussems ilicheza vizuri leo na kutengeneza nafasi nyingi, lakini tu ikakosa bahati ya kukwamisha mpira nyavuni.
   Dakika ya saba, kipa wa Lipuli FC, Mohammed Yussuph alilipoza kabla ya kulidaka shuti kali la Nahodha wa Simba SC.
  Dakika tatu baadaye Lipuli FC wakajibu na Miraji Athumani Madenge akapiga shuti kali baada ya kupokea pasi ya mshambuliaji mwenza, Paul Nonga lakini kipa wa Simba SC, Aishi Salum Manula akapangua na kutoka nje.
  Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na dakika ya 90 mshika kibendera namba moja, Charles Simon wa Dodoma alikataa bao la Simba SC lililofungwa kichwa na mshambuliaji Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere akimalizia krosi ya mtokea benchi Rashid Juma, akidai alikuwa ameotea. 
  Sifa zimuendee refa mwanamama, Florencina Zablon wa Dodoma aliyekuwa anasaidiwa na Charles Simon na Arnold Bugado wa Singida kwa kuumudu wa mchezo wa leo uliokuwa mkali na wa kusisimua..
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Paul Bukaba/James Kotei dk39, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/Haruna Niyonzima fk75, Cloutus Chama, Meddie kagere, John Bocco na Hassan Dilunga/Rashid Juma dk46. 
  Lipuli FC; Mohamed Yussuph, William Lucian ‘Gallas’, Paul Ngelema, Ibrahim Job/Novaty Lufunga dk62, Ally Sonso, Freddy Tangalu, Steven Mganga, Mussa Nampaka/Shaaban Ada dk66, Paul Nonga, Zawadi Mauya na Miraji Athumani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: REFA AKATAA BAO LA KAGERE DAKIKA ZA LALA SALAMA UWANJA WA TAIFA SIMBA SC YALAZIMISHWA SARE 0-0 NA LIPULI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top