• HABARI MPYA

  Wednesday, November 28, 2018

  MBARAKA YUSSUF APELEKWA KWA MKOPO NAMUNGO FC, MAHUNDI ASAINI MKATABA WA MIAKA MIWILI AZAM FC

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Azam FC imewatoa kwa mkopo wachezaji wake wanne, akiwemo mshambuliaji Mbaraka Yussuf Abeid aliyesajiliwa kwa msimu uliopita kutoka Kagera Sugar ya Bukoba.
  Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Iddi Maganga amesema kwamba Mbaraka Yussuf maarufu kwa jina la utani ‘Boban’ pamoja na Oscar Masai kwa pamoja wamepelekwa klabu ya Namungo FC ya Lindi inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.
  Aidha, Maganga amesema washambuliaji wengine, waliosajiliwa msimu uliopita pia, Waziri Junior kutoka Toto Africans ya Mwanza yeye amepelekwa kwa mkopo Biashara United ya Mara na Ditram Nchimbi aliyesajiliwa kutoka Njombe Mji FC amepelekwa Mwadui FC.

  Mbaraka Yussuf (kushoto) amepelekwa kwa mkopo Namungo FC ya Daraja kwa Kwanza

  Mbaraka Yussuf Abeid na Waziri Junior wote walisajiliwa Azam FC wakitakiwa na Yanga SC ya Dar es Salaam pia, lakini pamoja na kufuata maslahi mazuri Chamazi wameshindwa kuwavutia waajiri wao na sasa wanatupwa nje ya kikosi.
  Wakati huo huo kiungo wa timu hiyo Joseph Mahundi aliyesajiliwa misimu miwili iliyopita kutoka Mbeya City, ameongeza mkataba wa miaka miwili kuendelea kuitumikia klabu hiyo. 
  Wakati huo huo; kikosi cha Azam FC, kimeshaanza rasmi mazoezi leo tayari kuanza safari ya kuzisaka pointi kuelekea mchezo ujao dhidi ya Stand United.
  Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utafanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex Desemba 4 mwaka huu, ambapo Azam FC iko kwenye mwenendo mzuri baada ya kushinda mechi saba mfululizo za ligi hiyo.
  Wachezaji wote wa Azam FC wameripoti mazoezini wakiwa na hali nzuri kabisa isipokuwa kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambaye ni mgonjwa.
  Beki wa kulia Nickolas Wadada, aliyekuwa kwenye majukumu ya timu ya Taifa ya Uganda, naye amesharejea kundini akiwa ni miongoni mwa wachezaji walioripoti kwenye mazoezi hayo.
  Kikosi cha Azam FC kinatarajia kuendelea na mazoezi kwa wiki hii yote, Jumamosi hii asubuhi kikitarajia kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya vijana ya timu hiyo (Azam U-20) kwa ajili ya kujiweka sawa.
  Azam FC hadi sasa imeshacheza mechi 13 za ligi, ikiwa imesdhinda mara 10 na kutoka sare mara tatu ikijikusanyia jumla ya pointi 33 na kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MBARAKA YUSSUF APELEKWA KWA MKOPO NAMUNGO FC, MAHUNDI ASAINI MKATABA WA MIAKA MIWILI AZAM FC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top