• HABARI MPYA

  Jumapili, Novemba 18, 2018

  KILA LA LA HERI TAIFA STARS, MUNGU IBARIKI TIMU YETU ISHINDE LEO MASERU NA KUJIWEKA KWENYE NAFASI YA KUFUZU AFCON

  Na Mwandishi Wetu, MASERU
  TANZANIA inatarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa wa Setsoto mjini Maseru kumenyana na wenyeji, Lesotho katika mchzeo wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon.
  Katika mchezo huo utakaoanza Saa 11:00 jioni na kuonyeshwa na chaneli ya ZBC 2 inayopatikana kwenye kisimbusi cha Azam FC, Tanzania inahitaji ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu AFCON ya pili kihistoria kwake, baada ya ile ya mwaka 1980 nchini Nigeria.
  Na hiyo ni baada ya jana Uganda kuwa timu ya kwanza kufuzu AFCON ya mwakani Cameroon kutoka kundi hilo, kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya Cape Verde Uwanja wa Mandela, Namboole mjini Kampala, bao pekee la mshambuliaji wa KCCA ya nyumbani, Patrick Henry Kaddu dakika ya 78.

  Nahodha Mbwana Samatta aliyenyoosha mkono atakosekana leo, lakini bado Taifa Stars ina kikosi cha ushindi

  The Cranes inafikisha pointi 13 baada ya kucheza mechi ya tano, ikishinda nne na sare moja na kumaliza kileleni mwa Kundi L nyuma ya Tanzania, yenye pointi tano, Cape Verde pointi nne na Lesotho pointi moja.
  Katika mchezo wa leo, Tanzania itawakosa wachezaji wake wawili muhimu, Nahodha Mbwana Samatta anayechezea klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji ambayeb anatumikia adhabu ya kadi za njano na beki wa kulia wa Simba ya nyumbani, Shomari Kapombe ambaye ni majeruhi.
  Pamoja na Kapombe aliyewahi kuchezea AS Cannes ya Ufaransa, majeruhi mwingine Stars ni mshambuliaji wa BDF XI ya Botswana, Rashid Mandawa ambao wote waliumia siku mbili za mwisho kwenye kambi ya siku 10 mjini Bloemfontein, Afrika Kusini.
  Kuumia kwa Kapombe, mchezaji wa zamani wa Azam FC ni pigo kwa timu kutokana na kuwa mchezaji mwenye maarifa mengi mbali na uwezo wake na kiongozi pia wa wachezaji wenzake uwanjani, ingawa nafasi yake itazibwa na Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia.
  Kikosi cha Stars kinatarajiwa kuwa; Aishi Manula, Hassan Kessy, Gardiel Michael, Abdi Banda, Kelvin Yondan, Erasto Nyoni, Simon Msuva, Salum Abubakar, Feisal Salum, John Bocco na Shiza Kichuya.
  Katika benchi wanaweza kuwepo Beno Kakolanya, Ally ‘Sonso’ Abdulkarim, Aggrey Morris, Abdallah Kheri, Himid Mao, Mudathir Yahya, Salum Kimenya, Jonas Mkude, Shaaban Iddi Chilunda na Yahya Zayed.
  Kila la la heri Taifa Stars, mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki timu yetu ya taifa ifuzu AFCON. Amin. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KILA LA LA HERI TAIFA STARS, MUNGU IBARIKI TIMU YETU ISHINDE LEO MASERU NA KUJIWEKA KWENYE NAFASI YA KUFUZU AFCON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top