• HABARI MPYA

  Alhamisi, Novemba 29, 2018

  YANGA SC YAPANDA KILELENI LIGI KUU BAADA YA KUIPIGA JKT TANZANIA 3-0 SASA WANAWAZIDI SIMBA SC KWA POINTI SABA

  Na Nasra Omary, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imepanda kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa mara ya kwanza msimu huu, baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Tanzania jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Ushindi huo unaifanya Yanga SC kufikisha pointi 35 baada ya kucheza mechi 13, ikiwashusha nafasi ya Azam FC wenye pointi 33 za mechi 13 pia, wakati mabingwa watetezi, Simba SC wapo nafasi ya tatu kwa pointi zao 28 za mechi 13 pia.
  Ushindi wa leo wa Yanga SC inayofundishwa na kocha Mwinyi Zahera kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umetokana na mabao ya mshambuliaji Heritier Makambo na viungo Mrisho Ngassa na Ibrahim Ajibu.
  Nyota wa Yanga SC, Heritier Makambo (kulia) na Ibrahim Ajibu (kushoto) wakishangilia baada ya bao la kwanza
  Mfungaji wa bao la pili Yanga SC, Mrisho Ngassa akimtoka mchezaji wa JKT Tanzania
  Mfungaji wa bao la tatu la Yanga, Ibrahim Ajibu akiwatoka wachezaji wa JKT Tanzania

  Alianza Mkongo, Makambo kuifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 20 baada ya kuunasa mpira uliopotezwa na kiungo wa JKT Tanzania, Salim Aziz Gilla kabla na kumtoka beki Frank Nchimbi kabla ya kufumua shuti kutoka umbali wa mita zaidi ya 25.
  Akafuatia Mrisho Khalfan Ngassa kufunga bao la pili dakika ya 53 akifanya kazi nyepesi tu, kuubadili njia mpira uliopigwa na kiungo Raphael Daudi.
  Kipenzi cha wana Jangwani, Ibrahim Ajibu Migomba akaifungia Yanga SC bao la tatu dakika ya 79 kwa penalti baada ya Madenge Ramadhani kuunawa mpira kwenye boksi kufuatia shuti la mtokea benchi, kiungo Mzimbabwe, Thabani Scara Kamusoko.
  Yanga SC wangeweza kuondoka na ushindi mtamu zaidi kama wangetumia vyema nafasi zao nzuri waliotengeneza kwenye mchezo huo.
  Kipa chipukizi wa Yanga, Ramadhani Awam Kabwili alidaka kwa ustadi mkubwa leo na kuokoa michomo mingi iliyoelekezwa langoni mwake ukiwemo wa Gilla dakika ya 45, ambao ulionekana kuwa wa hatari zaidi.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ramadhani Kabwili, Paulo Godfrey, Mwinyi Mngwali, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Andrew Vincent ‘Dante’, Feisal Salum, Mrisho Ngassa/Cleophas Sospeter dk84, Raphael Daudi/Thabani Kamusoko dk73, Heritier Makambo, Ibrahim Ajibu na Deus Kaseke/Maka Edward dk46.
  JKT Tanzania; Abdulrahman Mohamed, Anuary Kilemile, Salim Gilla/Ally Billa dk49, Madenge Ramadhan, Frank Nchimbi, Mwinyi Kazimoto, Edward Songo, Daniel Mecha, Said Luyaya/ Idd Mbaga dk66, Hassan Materema na Abdalrahman Mussa/Kelvin Nashon dk62.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC YAPANDA KILELENI LIGI KUU BAADA YA KUIPIGA JKT TANZANIA 3-0 SASA WANAWAZIDI SIMBA SC KWA POINTI SABA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top