• HABARI MPYA

  Jumanne, Novemba 20, 2018

  MECHI YA SIMBA SC NA LIPULI ILIYOKUWA ICHEZWE KESHO UWANJA WA TAIFA IMESOGEZWA MBELE HADI IJUMAA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MCHEZO wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kati ya wenyeji, Simba SC na Lipuli FC uliopangwa kufanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam umesogezwa mbele hadi Ijumaa.
  Mabadiliko hayo yamefanywa ili kuwapa mapumziko nafasi wachezaji wa Simba na Lipuli waliokuwa kwenye timu zao za Taifa kujiunga na vikosi vyao.
  Lipuli FC inayofundishwa na kocha Suleiman Abdallah Matola ilikuwa na mchezaji mmoja tu kwenye timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilichofungwa 1-0 na Lesotho Jumapili mjini Maseru katika mchezo wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon.
  Lakini Simba SC ilikuwa ina wachezaji sita ambao ni kipa Aishi Manula, mabeki Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, viungo Jonas Mkude, Shiza Kichuya na mshambuliaji John Bocco.

  Pamoja na wachezaji wengine wanne wa kigeni wa Simba SC walikuwa na timu za taifa ambao ni beki Juuko Murshid, washambuliaji Emmanuel Okwi wa Uganda, Meddie Kagere wa Rwanda na kiungo Cloutus Chama wa Rwanda.  
  Ligi Kuu itaendelea Alhamisi kwa mchezo mmoja tu, Yanga SC wakiwa wageni wa Mwadui FC Uwanja wqa CCM Kambarage mjini Shinyanga kuanzia Saa 10: 00 jioni.
  Yanga SC watakuwa na mechi mbili zaidi kabla ya mwisho wa mwezi, Jumapili wakimenyana na Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na Novemba 29 wakiifuata JKT Tanzania Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
  Kuna uwezekano sasa mchezo mwingine wa Simba SC dhidi ya Biashara United uliopangwa kufanyika Jumapili kuanzia Saa 10: 00 jioni mjini Dar es Salaam nao ukasogezwa mbele.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MECHI YA SIMBA SC NA LIPULI ILIYOKUWA ICHEZWE KESHO UWANJA WA TAIFA IMESOGEZWA MBELE HADI IJUMAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top