• HABARI MPYA

  Jumapili, Novemba 25, 2018

  YANGA SC YAENDELEA KUKUSANYA POINTI MIKOANI, YAIPIGA KAGERA SUGAR 2-1 NA KUISOGEELA KABISA AZAM FC KILELENI

  Na Mwandishi Wetu, BUKOBA
  YANGA SC imeisogelea Azam FC kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji, Kagera Sugar jioni ya leo Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
  Kwa ushindi huo, Watoto hao wa Jangwani wanafikisha pointi 32 baada ya kucheza mechi 12, sasa wakizidiwa pointi moja tu na Azam FC ya Dar es Salaam pia, ambayo hata hivyo imecheza mechi moja zaidi. 
  Yanga SC, sasa wanawazidi kwa pointi tano mabingwa watetezi, Simba SC ambao wana pointi 27 baada ya kucheza mechi 12 pia.

  Kikosi cha Yanga SC kilichoanza leo Uwanja wa Kaitaba na kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Kagera Sugar

  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Jacob Adongo, Yanga SC walitangulia kwa bao la mshambuliaji wake Heritier Makambo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) dakika ya 21 aliyefunga kwa kichwa akimalizia krosi maridadi ya beki wa kushoto, Mwinyi Hajji Mngwali aliyepokea pasi ya Mrisho Ngassa.
  Na Kagera Sugar inayofundishwa na kocha Mecky Mexime Kianga ikasawazisha kwa penalti, mfungaji Ramadhani Kapera dakika ya 32 baada ya Edward Christopher aliyewazidi mbio mabeki wa Yanga kuangushwa na kipa Ramadhani Kabwili.
  Kipindi cha pili kocha wa Yanga SC, Mwinyi Zahera alianza na mabadiliko mfululizo akiwapumzisha kwanza Mkongo mwenzake, Heritier Makambo na kumuingiza Ibrahim Ajib na baadaye akiwatoa Maka Edward na Mwinyi Hajji Mngwali na kuwaingiza Raphael Daudi na Deus Kaseke.
  Mabadiliko hayo yaliwasaidia mabingwa hao mara nyingi zaidi wa Ligi Kuu kihistoria kupata bao la ushindi dakika ya 74 mfungaji Raphael Daudi kwa kichwa akimalizia mpira uliosogezwa kwa kichwa pia na mtokea benchi mwenzake, Deus Kaseke baada ya krosi ya beki wa kulia, Paulo Godfrey.
  Kikosi cha Kagera Sugar kilikuwa; Said Kipao, Mwaita Gereza, David Luhende, Ahmad Waziri, Juma Nyosso/Juma Shemvuni dk30, Majjid Khamis, Japhet Makalai, Peter Mwalyanzi, Ramadhani Kapera, Ally Ramadhani na Edward Christopher.
  Yanga SC; Ramadhani Kabwili, Paulo Godfrey, Mwinyi Mngwali/Deus Kaseke dk60, Andrew Vincent ‘Dante’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Feisal Salum, Mrisho Ngassa, Maka Edward/Raphael Daudi dk50, Heritier Makambo/Heritier Makambo dk46, Matheo Anthony na Jaffar Mohammed.
  Mrisho Ngassa akimpongeza Heritier Makambo (kulia) baada ya kufunga bao la kwanza 
  Daktari wa Yanga, Edward Bavu akimpatia matibabu mshambuliaji Matheo Anthony
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC YAENDELEA KUKUSANYA POINTI MIKOANI, YAIPIGA KAGERA SUGAR 2-1 NA KUISOGEELA KABISA AZAM FC KILELENI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top