• HABARI MPYA

  Jumamosi, Novemba 17, 2018

  SALAH AFUNGA DAKIKA YA MWISHO MISRI YAICHAPA TUNISIA 3-2

  MSHAMBULIAJI Mohamed Salah jana amefunga bao la dakika ya mwisho kuisaidia Misri kutoka nyuma na kushinda 3-2 dhidi ya Tunisia katika mchezo wa Kundi J Kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria.
  Morocco iliifunga Cameroon 2-0 mjini Casablanca na sasa wanahitaji pointi moja kujihakikishia nafasi ya kwenda fainali za mwakani, wakati Burundi imekaribia kufuzu kwa mara ya kwanza baada ya ushindi wa 5-2 ugenini dhidi ya Sudan Kusini.
  Misri na Tunisia tayari zimefuzu kutoka Kundi J, lakini mchezo baina yao ulikuwa una upinzani mkali hususan baada ya Esperance ya Tunisia kuinyuka Al Ahly ya Misri na kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika.

  Naim Sliti alianza kuifungia Tunisia dakika ya 13 kabla ya Misri kusawazisha kupitia kwa Mahmoud 'Trezeguet' Hassan.
  Baher El Mohamady akaifungia Misri bao la pili dakika ya 59, lakini beki mwenzake Ahmed Hegazi akampa nafasi Sliti kuifungia tena Tunisia zikiwa zimesalia dakika tano kabla ya Salah kufunga la ushindi dakika ya 90 na ushei.
  Tunisia inaendelea kuongoza kwa hesabu za matokeo ya jumla ya mechi baina yao, baada ya timu zote kujikusanyia pointi 12 katika mechi tano ilizocheza. Misri sasa imeshinda mechi nne tangu baada ya Kombe la Dunia chini ya kocha mpya, Javier Aguirre.
  Hat-trick ya Abdul Razak Fiston ikaisaidia Burundi katika ushindi wa 5-2 dhidi ya wenyeji, Sudan Kusini mjini Juba na kupanda kileleni mwa Kundi C ikifikisha pointi tisa katika mechi ya tano.
  Mali, yenye pointi nane, na Gabon, saba, zitakutana mjini  Libreville leo.
  Burundi, iliyoongezewa nguvu na mshambuliaji Saido Berahino aliyeamua kuitumikia timu ya nyumbani badala ya England, watahitaji ushindi wa ugenini katika mchezo wa mwisho dhidi ya Gabon mwezi Machi mwakani kufuzu AFCON ya Cameroon.
  Berahino na Cedric Hamissi pia waliifungia Burundi mabao mengine, huku Atak Lual na Dominic Aboy Koni wakifunga mabao ua Sudan Kusini inayoendelea kuwa haina pointi.
  Hakim Ziyech aliifungia Morocco dakika ya 54 kwa penalti na lingine kwa shuti la kutokea nje ya boksi dakika 12 baaadaye kuipa ushindi timu yake dhidi ya Cameroon mjini Casablanca.
  Cameroon wanacheza mechi za kufuzu licha ya kwamba wao ni wenyeji wa AFCON ya mwakani ili tu kuongeza uhondo wa mashindano, lakini wamekwishafuzu moja kwa moja.
  Mechi za kufuzu AFCON ziatarajiwa kuendelea leo na kesho kusak timu za kuungana na Cameroon, Misri, Madagascar, Senegal na Tunisia katika fainali zitakazoshirikisha timu 24.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SALAH AFUNGA DAKIKA YA MWISHO MISRI YAICHAPA TUNISIA 3-2 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top