• HABARI MPYA

  Alhamisi, Novemba 22, 2018

  KESI YA AKINA MALINZI YAAHIRISHWA HADI DESEMBA 5 KWA SABABU WAKILI WA SERIKALI ALIKUWA ANA SHUGHULI NYINGINE LEO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KESI inayowakabili vigogo wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), aliyekuwa Rais Jamal Malinzi na wenzake wane imeahirishwa hadi Desemba 5, mwaka huu kutokana na Wakili wa Serikali, Leonard Swai anayeendesha shauri hilo kuwa na shughuli nyingine za kiofisi.
  Washitakiwa wote walipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, wakati shauri lilipotajwa kwa ajili ya kuendelea na ushaidi upande wa mashitaka.
  Wakili wa Serikali Pendo Temu, aliomba mahakama tarehe nyingine ya kutajwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji upande wa mashitaka.
  "Naiomba mahakama kuahirisha shauri hilo kwani Wakili Swai amekuwa na shughuli nyingine za kiofisi," alidai.
  Baada ya hoja hiyo, Wakili wa utetezi Richard Rweyongeza, alikubaliana na ombi hilo ambapo aliomba mahakama shauri hilo lipangiwe tarehe ya karibu hata kama iwe leo.
  Hakimu Mashauri  alikubaliana na ombi hilo ambapo aliahirisha shauri hilo hadi Desemba 5, mwaka huu kwa kuendelea ambapo washitakiwa walirudishwa rumande.
  Mbali na aliyekuwa rais TFF, Jamal  Malinzi(57) wengine ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Joas Selestine(46) na Mhasibu wa TFF,  Nsiande Isawayo Mwanga(27).
  Meneja wa  Ofisi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya ambao Kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 30 katika   kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa USD 173,335 na sh. 43,100,000.
  Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wapo rumande kwa kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji wa fedha kuwa miongoni mwa mashtaka  ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana huku wenzao Miriam na Flora wapo nje kwa dhamana.
  Katika kesi hiyo tayari mashahidi wanane wa upande wa mashitaka wamekwishatoa ushahidi kwenye kesi hiyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KESI YA AKINA MALINZI YAAHIRISHWA HADI DESEMBA 5 KWA SABABU WAKILI WA SERIKALI ALIKUWA ANA SHUGHULI NYINGINE LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top