• HABARI MPYA

  Jumamosi, Novemba 17, 2018

  CHIRWA AFUNGUA AKAUNTI YA MABAO AZAM FC AKICHEZA MECHI YA KWANZA TU TIMU IKISHNDA 2-0 DHIDI YA U23 YA TANZANIA

  Na Saada Salmin, DAR ES SALAAM
  AKICHEZA mechi yake ya kwanza tokea asajiliwe na Azam FC, mshambuliaji Obrey Chirwa, amefungua akaunti ya mabao kwa kufunga moja wakati timu hiyo ikiilaza timu ya Taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 23 (Ngorongoro Heroes) mabao 2-0.
  Mchezo huo wa kirafiki umefanyika Uwanja wa Azam Complex usiku huu, Ngorongoro Heroes ikiutumia kama sehemu ya maandalizi kuelekea mchezo wa marudiano dhidi ya vijana wenzao wa Burundi.
  Azam FC ilipata bao la uongozi dakika ya 12 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na winga Enock Atta, ambaye kwenye mchezo huo alicheza kama kiungo mchezeshaji, penalti hiyo ilipatikana baada ya Ramadhan Singano ‘Messi’, kuangushwa ndani ya eneo la hatari.
  Mshambuliaji mpya wa Azam FC, Mzambia Obrey Chirwa (kulia) akimtoka beki wa U23 ya Tanzania leo 
  Beki na Nahodha wa U23 ya Tanzania, Abdallah Shaibu 'Ninja'  akiwa chini kuokoa dhidi ya mshambuliaji Mzimbabwe wa Azam FC, Donald Ngoma
  Nahodha Abdallah Shaibu 'Ninja' (kulia) akimdhibiti mshambuliaji wa Azam FC, Iddi Kipagwile
  Beki Mghana, Yakubu Mohammed akimiliki mpira mbele ya mshambuliaji wa U23 ya Tanzania

  Ngorongoro inayofundishwa na Kocha Bakari Shime, ilionekana kucheza vema hasa kipindi cha pili, ikijaribu kila wakati kusaka bao la kusawazisha lakini safu ngumu ya ulinzi ya Azam FC ilisimama vema kuondosha hatari zote.
  Chirwa aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Donald Ngoma, alianza vema kibarua chake kwenye mechi yake ya kwanza kuvaa uzi wa Azam FC akifanya jitihada kubwa dakika ya 88 kwa kufunga bao safi na kuihakikishia ushindi timu yake.
  Mshambuliaji huyo wa zamani wa Platinum ya Zimbabwe, Yanga na Nagoon FC ya Misri, alifunga bao hilo akiungaisha pande safi la juu lililopigwa na aliyekuwa Nahodha kwenye mchezo huo, Yakubu Mohammed.
  Benchi la ufundi la Azam FC liliutumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi kuelekea mchezo wake ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) dhidi ya Ruvu Shooting Novemba 22 mwaka huu.
  Hadi sasa wakati ligi hiyo ikitarajia kuendelea kuanzia Jumatano ijayo, Azam FC ipo kileleni baada ya kufikisha jumla ya pointi 30 baada ya kushinda mechi tisa na sare tatu ikiwa haijapoteza hata mmoja na ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu.
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ally, Lusajo Mwaikenda, Bruce Kangwa/Hassan Mwasapili dk 46, David Mwantika, Yakubu Mohammed (C), Salmin Hoza, Idd Kipagwile/Emmanuel dk 74, Enock Atta/Abubakar Kambi, Donald Ngoma/Chirwa dk 46, Danny Lyanga, Ramdhan Singano/Novatus dk 79
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: CHIRWA AFUNGUA AKAUNTI YA MABAO AZAM FC AKICHEZA MECHI YA KWANZA TU TIMU IKISHNDA 2-0 DHIDI YA U23 YA TANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top