• HABARI MPYA

  Wednesday, November 28, 2018

  SIMBA SC YATOA ONYO AFRIKA, YAITANDIKA MBABANE SWALLOWS 4-1 LIGI YA MABINGWA BOCCO AFUNGA MABAO MAWILI

  Na Saada Salmin, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Simba SC imeanza vyema michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 4-1 kwenye mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali dhidi ya Mbabane Swallows ya Eswatini, zamani Swaziland jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Ushindi huo unamaanisha Simba SC imerahisisha kazi kuelekea mchezo wa marudiano Desemba 4 nchini Swaziland, kwani wenyeji watatakiwa kushinda 3-0 ili kusonga mbele.
  Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa, Pacifique Ndabihawenimana aliyesaidiwa na washika vibendera Willy Habimana na Gustave Baguma wote wa Burundi, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-1.
  Nahodha John Bocco (kulia) leo amefunga mabao mawili katika ushindi wa Simba SC 4-1

  John Bocco akiwa ametoa pasi mbele ya mchezaji wa Mbabane Swallows leo Uwanja wa Taifa

  Wachezaji wa Simba SC wakimpongeza mwenzao, Cltous Chama baada ya kufunga bao la nne
  Clatous Chama akipasua katikati ya wachezaji wa Mbabane Swallows leo 
  Meddie Kagere akipiga shuti mbele ya beki wa Mbabane Swallows leo  
  Mmiliki wa Simba SC, Mohammed 'Mo' Dewji akifurahia baada ya bao la nne Uwanja wa Taifa
  Na mabao yote ya Simba SC yalifungwa na Nahodha wake, John Raphael Bocco dakika ya nane, akimalziia pasi ya beki Mghana, Asamoah Gyan kutoka upande wa kulia na la pili kwa penalti dakika ya 33 kwa penalti baada ya mshambuliaji Uganda, Emmanuel Arnold Okwi kudondoshwa ndani ya boksi.
  Na Bocco alifunga bao la pili baada ya Mbabane Swallows kusawazisha dakika ya 24 kwa bao la Guevane Nzambe aliyefumua shuti kutoka nje ya boksi.
  Kipindi cha pili, kocha Mbelgiji Patrick J Aussems akabadilisha mbinu na Simba SC ikafanikiwa kuunenepesha ushindi wake.
  Mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere akaifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 84 akiuwahi mpira baada ya kipa wa Mbabane Swallows, Sandanezwe Mathabela kuteleza na kufunga kiulaini.
  Kiungo Mzambia, Clatous Chama akakamilisha shangwe za mabao za Wekundu wa Msimbazi baada ya kufunga bao la nne dakika ya 90 na ushei, akimalizia pasi nzuri ya kiungo Hassan Dilunga aliyetokea benchi zikiwa zimesalia dakika tatu.
  Mapema kabla ya mchezo huo, Simba SC ilitangaza kumleta beki Zana Coulibaly kutoka ASEC Mimosas ya Ivory Coast leo kwa ajili kukamilisha taratibu za mwisho kujiunga na timu hiyo kuziba pengo la Shomari Kapombe ambaye ni majeruhi. 
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Nicholas Gyan, Mohammed Hussein, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, James Kotei, Clatous Chama, Jonas Mkude, John Bocco/Hassan Dilunga dk87, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi/Shiza Kichuya dk60. 
  Mbabane Swallows; Sandanezwe Mathabela, Tony Tsabedze, Richard Sewu, Gueyane Nzambe, Joseph Ndaba, Siboniso Nzabanbaba, Colani Sikhondze, Njabulo Ndlovu, Wonder Nhleko, Selliey Tarawallie/ Sirowethu Shabalala dk57 na Sandile Hlatswako.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YATOA ONYO AFRIKA, YAITANDIKA MBABANE SWALLOWS 4-1 LIGI YA MABINGWA BOCCO AFUNGA MABAO MAWILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top