• HABARI MPYA

  Sunday, November 18, 2018

  YANGA SC YALAZIMISHWA SARE YA 1-1 NA NAMUNGO FC MBELE YA WAZIRI MKUU WA NCHI, KASSIM MAJALIWA RUANGWA

  Na Mwandishi Wetu, RUANGWA
  TIMU ya Yanga SC leo imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, Namungo FC katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Majaliwa mjini Ruangwa mkoani Lindi.
  Sare hiyo inamaamanisha vigogo wote wa soka nchini wameshindwa kuifunga timu hiyo ya Daraja la Kwanza, baada ya Agosti mwaka huu, Simba SC nayo kulazimishwa sare ya 0-0 Agosti 11, mwaka huu hapo hapo Ruangwa.
  Katika mchezo huo ambao mgeni Rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Yanga SC ilitangulia kupata bao kupitia kwa beki wake wa kati, Andrew Vincent Chikupe ‘Dante’ dakika ya 54 kwa kichwa akimalizia krosi ya winga Deus Kaseke.
  Nahodha wa Yanga SC, Juma Abdul akimtambulisha mgeni, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa (kulia) kwa wachezaji wenzake leo 
  Wachezaji wa Yanga wakimpongeza mwenzao, Andrew Vincent 'Dante' baada ya kufunga leo  

  Wachezaji wa Yanga SC na Namungo FC wakipeana mikono baada ya mechi leo 

  Lakini makosa ya safu ya ulinzi yakawapa Namungu FC bao la kusawazisha dakika ya 84, mfungaji akiwa mchezaji wa zamani wa Yanga, Loriant Lusako aliyemchambua kipa kipa Klaus Kindoki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Lakini Yanga SC watajilaumu wenyewe kwa kushindwa kupata ushindi kwenye mchezo wa leo, kwani walitengeneza nafasi nyingine wakashindwa kuzitumia, huku mshambuliaji Mkongo Heritier Makambo akikosa bao la wazi zaidi baada ya kuingia kipindi cha pili. 
  Kindoki leo ameidakia Yanga SC kwa mara ya nane tangu asajiliwe Julai mwaka huu na kufungwa bao la tano. 
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Klaus Kindoki, Juma Abdul, Gustavo Simon, Cleophas Sospeter, Andrew Vincent ‘Dante’, Maka Edward/Said Juma ‘Makapu’ dk77, Deus Kaseke/Mrisho Ngassa dk65, Thabani Kamusoko/Raphael Daudi dk75, Yohanna Nkomola/Amissi Tambwe dk58, Yussuf Mhilu/Heritier Makambo dk58 na Emmanuel Martin/Matheo Anthony dk65.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YALAZIMISHWA SARE YA 1-1 NA NAMUNGO FC MBELE YA WAZIRI MKUU WA NCHI, KASSIM MAJALIWA RUANGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top