• HABARI MPYA

  Jumapili, Novemba 18, 2018

  TANZANIA YACHAPWA 1-0 NA LESOTHO NA KUPUNGUZA MATUMAINI YA KUFUZU AFCON YA MWAKANI CAMEROON

  Na Mwandishi Wetu, MASERU
  MATUMAINI ya Tanzania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) mwakani yameanza kufifia tena baada ya kuchapwa bao 1-0 na wenyeji, Lesotho jioni ya leo Uwanja wa Setsoto mjini Maseru.
  Bao lililoizamisha Taifa Stars leo limefungwa na beki wa klabu ya Matlama Maseru, Nkau Lerotholi dakika ya 76 kwa kichwa akimalizia mpira wa kona kutoka upande wa kulia.  
  Kwa matokeo hayo, sasa timu yoyote kati ya tatu, Lesotho, Tanzania na Cape Verde zinaweza kuungana na vinara wa kundi hilo, Uganda kwenda Cameroon katikati ya mwaka ujao.
  Mamba wa Lesotho wanapanda nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi tano sawa na Tanzania, wakati Cape Verde inashika mkia kwa pointi zake nne.

  Lesotho ikiifunga Cape Verde Machi mwakani itafuzu AFCON hata kama Tanzania itaifungaje Uganda mjini Dar es Salaam kwa sababu ya matokeo ya mechi zilizohusisha timu zilizofungana kwa pointi.
  Cape Verde nayo itafuzu ikiifunga Lesotho na Tanzania ikalazimishwa sare ya Uganda. Taifa Stars inaweza kufuzu iwapo itaifunga Uganda na Cape Verde ikashinda au kutoa sare na Lesotho katika mechi za mwisho.   
  Dalili za Taifa Stars kupoteza mechi ya leo zilianza kuonekana mapema tu kutokana na kuzidiwa na wenyeji na kuanza kukoswa mabao ya wazi mapema.
  Lakini upangwaji wa kikosi na mfumo wa kujihami wa kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike aliyewaacha benchi wachezaji wazoefu akiwemo mshambuliaji John Raphael Bocco aliyepewa nafasi kubwa ya kuanza, navyo vilichangia.
  Aidha, kuwachezesha wachezaji nje ya nafasi zao nako kuliipa mzigo mzito timu leo kupata matokeo mazuri iliyotahitaji.
  Kikosi cha Lesotho kilikuwa; Samuel Khetsekile, Mafa Moremoholo, Basia Makepe, Bokang Sello, Tsoarelo Bereng/Hlompho Kalake dk71, Tsepo Toloane, Thapelo Tale/Sera Motebang dk51, Sepiriti Malefane, Jane Thaba-Ntso/Jane Tsotleko dk70, Tumelo Khutlang na Nkau Lerotholi.
  Tanzania; Aishi Manula, Abdallah Kheri/John Bocco dk83, Ally Sonso, Aggrey Morris, Kelvin Yondan, Erasto Nyoni, Mudathir Yahya/Feisal Salum ‘Fei Toto’dk73, Himid Mao, Simon Msuva, Shaaban Iddi Chilunda na Gardiel Michael/Shiza Kichuya dk59.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TANZANIA YACHAPWA 1-0 NA LESOTHO NA KUPUNGUZA MATUMAINI YA KUFUZU AFCON YA MWAKANI CAMEROON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top