• HABARI MPYA

  Alhamisi, Novemba 22, 2018

  YANGA SC YAREJEA JUU YA SIMBA KWENYE MSIMAMO WA LIGI KUU BAADA YA KUITANDIKA MWADUI FC 2-1 LEO SHINYANGA

  Na Mwandishi Wetu, SHINYANGA
  YANGA SC imerufi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji, Mwadui FC Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga jioni ya leo.
  Yanga SC inafikisha pointi 29 baada ya kucheza mechi 11, sasa ikiwazidi kwa pointi tatu mabingwa watetezi, Simba SC waliocheza mechi 11 pia – wote wakiwa nyuma ya Azam FC yenye pointi 30 za mechi 12.
  Shukrani kwa mfungaji wa bao la ushindi katika mchezo wa leo, Mrisho Khalfan Ngassa dakika ya 55 kwa shuti kali baada ya kupata pasi ya Matheo Anthony kufuatia mpira wa adhabu wa kiungo Feisal Salum.
  Na Ngassa alifunga bao hilo mwanzoni mwa kipindi cha pili, baada ya timu kumaliza dakika 45 za kwanza zikiwa zimefungana 1-1.

  Ni Yanga SC waliotangulia kupata bao dakika ya tisa, mfungaji mshambuliaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Heritier Makambo dakika ya tisa tu akiwahadaa mabeki wa Mwadui na kupiga shuti kali baada ya pasi ya Paulo Godfrey.
  Mwadui FC walipambana baada ya bao hilo hadi kuja kufanikiwa kusawazisha nusu saa baadaye, mfungaji Salim Aiyee aliyemalizia mpira uliotemwa na kipa Mkongo wa Yanga, Klaus Kindoki baada ya shuti la Charles Ilamfya.  
  Kipindi cha kwanza timu hizo zilishambuliana kwa zamu na kipindi cha pili, Yanga SC walicheza vizuri zaidi hususan baada ya mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mkongo, Mwinyi Zahera akiwatoa kipa Kindoki, beki Gardiel Michael na mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe na kuwaingiza wazawa kipa Ramadhani Kabwili, kiungo Raphael Daudi na mshambuliaji Matheo Anthony. 
  Mechi nyingine ya Ligi Kuu inafuatia sasa, Azam FC ikiwakaribisha Ruvu Shooting ya Pwani kuanzia Saa 1:00 usiku Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam. 
  Kikosi cha Mwadui FC kilikuwa; Revocatus Richard, Miraj Maka, Frank Magingi, Joram Mgeveke, Leonard Ernest, Jean Marie Girukwishaka, Abdallah Seseme, Charles Ilamfya, Salim Aiyee, Ottu Samuel/John Kasanzu dk62.
  Yanga SC; Klaus Kindoki/Ramadhani Kabwili dk46, Paul Godfrey, Gardiel Michael/Matheo Anthony dk46, Andrew Vincent ‘Dante’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Feisal Salum, Mrisho Ngassa, Maka Edward, Heritier Makambo, Amissi Tambwe/Raphael Daudi dk61 na Jaffar Mohammed.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC YAREJEA JUU YA SIMBA KWENYE MSIMAMO WA LIGI KUU BAADA YA KUITANDIKA MWADUI FC 2-1 LEO SHINYANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top