• HABARI MPYA

  Jumanne, Novemba 20, 2018

  YANGA SC WAIFUATA MWADUI FC KWA NDEGE MECHI NI ALHAMISI UWANJA WA KAMBARAGE MJINI SHINYANGA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIKOSI cha Yanga SC kimeondoka Alfajiri ya leo kwa ndege kwenda Mwanza kuunganisha usafiri wa barabara kwenda Shinyanga kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Mwadui FC Alhamisi Saa 10:00 jioni Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.
  Yanga SC inaondoka siku moja tu baada ya kurejea jana Dar es Salaam kutoka Lindi, ambako juzi ilicheza mechi ya kirafiki na kutoa sare ya 1-1 na wenyeji, Namungo FC Uwanja wa Majaliwa huko Ruangwa.
  Wachezaji wote wa Yanga SC wakiwemo waliokuwa na timu za taifa wamesaifiri na ndege ya shirika la Tanzania (ATC) kwa ajili ya mchezo huo ambao utakuwa wa 11 wa msimu kwao.

  Wachezaji wa Yanga SC, Mrisho Ngassa (kulia) na Ibrahim Ajib (kushoto) baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Mwanza tayari kuunganisha usafiri wa Shinyanga

  Kocha Mwinyi Zahera amerejea kutoka kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) alipokwenda kwa majukumu ya timu yake ya taifa lakini hajasafiri na timu na ataungana nao kesho amebaki Dar es Salaam kwa mapumziko. 
  Kwa ujumla Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea kesho baada ya kusimama kupisha mechi za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon.
  Na mabingwa watetezi, Simba SC watakuwa wenyeji wa Lipuli FC Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kuanzia Saa 12:00 jioni.
  Vigogo hao wote watarudi kazini Jumapili, Yanga SC wakiwa wageni wa Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na Simba SC wakiwa wenyeji wa Biashara United ya Mara Uwanja wa Taifa, mecho zote zikianza Saa 10: 00 jioni.
  Yanga SC watateremka tena dimbani Novemba 29 kumenyana na JKT Tanzania Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga kiuanzia Saa 10: 00 jioni kukamilisha mechi za mwezi huu za Ligi Kuu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC WAIFUATA MWADUI FC KWA NDEGE MECHI NI ALHAMISI UWANJA WA KAMBARAGE MJINI SHINYANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top