• HABARI MPYA

  Thursday, November 22, 2018

  ABDI BANDA ASEMA KUCHEZA TIMU YA TAIFA NI HESHIMA KWA MCHEZAJI, HATASUSA KWA KUWEKWA BENCHI NA AMUNIKE

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BEKI wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Hassan Banda amesema kwamba hana ndoto za kususa kuchezea timu ya taifa kwa sababu ni fahari kwa mchezaji.
  Banda amelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kuenezwa ujumbe kwamba hatachezea tena Taifa Stars hadi kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike amalize muda wake.
  Hiyo ni baada ya Amunike kumuweka benchi beki huyo wa Baroka FC ya Afrika Kusini katika mchezo wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Lesotho Jumapili, Tanzania ikifungwa 1-0 mjini Maseru.
  “Mimi nitachezea Taifa Stars, labda nisiitwe. Na kucheza timu ya taifa ni heshima kwa sisi tunaocheza hivi vitimu vidogo huku nje,”amesema beki huyo wa zamani wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam.

  Abdi Banda (kushoto) akiwa na kocha wake wa zamani Simba SC, Dylan Kerr wiki hii walipokutana wakiwa safarini pamoja

  Banda amesema kwamba maneno mengi yanasemwa baada ya Taifa Stars kufungwa na Lesotho Jumapili na kila mtu anasema lake, lakini kikubwa yeye hakupewa nafasi kutokana na ubora wa wachezaji waliopangwa badala yake ambao waliouonyesha mazoezini na kumridhisha kocha.
  Banda aliye katika msimu wake wa pili Baroka FC tangu asajiliwe kutoka Simba SC ambayo nayo ilimtoa Coastal Union ya Tanga, amesema kwamba kocha Amunike ndiye mwenye haki ya kuchagua mchezaji wa kucheza kwenye timu. 
  “Kitendo cha kuanza kuandika au kudanganya Watanzania nimemshauri mwalimu kuhusu wachezaji, bado sijawa na uwezo huo, maana kuna walimu zaidi ya wane, wana kazi gani pale?,”. 
  “Na mwalimu akisema tucheze mabeki 11, tutacheza labda kuna kitu kakiona, sasa haya maneno sijui nimejitoa timu ya taifa yanatoka wapi, au ni kuanza kupandikiza chuki dhidi yangu na walimu na Watanzania ikiwa najijua sipendezwi kwa baadhi ya watu,”amesema na kuongeza; “Kikubwa tujue tumekosea wapi, ila hizi chuki hazijengi na usijaribu kuharibu maisha ya mwenzako,”. 
  Abdi Bandf akiwa na wachezaji wenzake wa Taifa Stars wanaocheza nje kulia ni Simon Msuva wa Difaa Hassan El Jadidi ya Morocco, Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana na Rashid Mandawa wa CD Tenerife ya Hispania (kushoto) 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ABDI BANDA ASEMA KUCHEZA TIMU YA TAIFA NI HESHIMA KWA MCHEZAJI, HATASUSA KWA KUWEKWA BENCHI NA AMUNIKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top