• HABARI MPYA

  Friday, November 30, 2018

  AKINA SAMATTA WATOA SARE 2-2 UGENINI YA EUROPA LEAGUE, LAKINI BADO WANAENDELEA KUONGOZA KUNDI LAO

  Na Mwandishi Wetu, MALMO
  NAHODHA wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana amecheza kwa dakika 73 timu yake, KRC Genk ikitoa sare ya kufungana mabao 2-2 na wenyeji Malmo FF katika mchezo wa Kundi I Europa League Uwanja wa Swedbank mjini Malmo, Sweden.
  Sare inaifanya Genk ifikishe point inane na kuendelea kuongoza kundi hilo kuelekea mechi za mwisho wiki ijayo, ikifuatiwa na Besiktas ya Uturuki yenye pointi saba, Malmo FF pointi sita na Sarpsborg 08 pointi tano.
  Genk sasa watahitaji ushindi katika mchezo wa mwisho dhidi ya Sarpsborg 08 nyumbani Desemba 13 ili kusonga mbele kwenye hatua ya mtoano ya michuano hiyo.
  Katika mchezo wa jana, Genk walifanikiwa kuongoza 2-0 kwa muda mrefu, kazi nzuri ya kiungo Mspaniola, Alejandro Pozuelo Malero aliyefunga bao la kwanza dakika ya 42 akimalizia pasi ya Leandro Trossard kabla ya kumsetia mshambuliaji kutoka Ghana, Joseph Paintsil kufunga la pili dakika ya 53.
  Mbwana Samatta akiwania mpira wa juu dhidi ya beki wa Malmo FF, Behrang Safari raia wa Tehran jana Uwanja wa Swedbank mjini Malmo 

  Mbwana Samatta nyuma kabisa akimuangalia mchezaji mwezake, akimtoka kiungo Mcomoro wa Malmo FF, Fouad Bachirou mzaliwa wa Ufaransa 

  Lakini wenyeji wakacharuka na kusawazisha ndania ya dakika mbili kuanzia dakika ya 65 akianza kiungo, Oscar Lewicki akifuatiwa na mshambuliaji Marcus Antonsson dakika ya 67, wote Wasweden.
  Samatta jana amecheza mechi ya 131 katika mashindano yote tangu amejiunga na KRC Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akiwa jumla ya mabao 51.
  Katika Ligi ya Ubelgiji pekee amefikisha mechi 101 na kufunga mabao 36, Kombe la Ubelgiji mechi nane na mabao mawili na Europa League mechi 22 mabao 14.
  Kikosi  cha Malmo FF kilikuwa; Dahlin, Safari/Brorsson dk83, Rieks, Lewicki, Bachirou, Traustason/Antonsson dk54, Rosenberg, Christiansen/Gall dk83, Bengtsson, Nielsen na Vindheim.
  KRC Genk; Vukovic, Maehle, Aidoo, Dewaest, Uronen, Berge, Malinovskyi, Pozuelo/Heynen dk86, Paintsil/Ndongala dk54, Trossard na Samatta/Gano dk72.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AKINA SAMATTA WATOA SARE 2-2 UGENINI YA EUROPA LEAGUE, LAKINI BADO WANAENDELEA KUONGOZA KUNDI LAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top