• HABARI MPYA

  Ijumaa, Novemba 16, 2018

  SIMBA SC YAONYESHA NI TISHIO, YATOA SARE NA BIG BULLETS LICHA YA KUWAKOSA NYOTA WAKE KIBAO WA KIKOSI CHA KWANZA

  Na Nasra Omary, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imedhihirisha siyo tu ina kikosi kipana, lakini pia imara baada ya kutoa sare ya 0-0 na Nyasa Big Bullets ya Malawi katika mchezi wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Pamoja na kuwakosa karibu wachezaji wake wote wa kikosi cha kwanza ambao wamechukuliwa na timu zao za taifa kwa ajili ya mechi za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ya wakubwa na ya vijana chini ya umri wa miaka 23, Simba ilicheza vyema na kukaribia kushinda.   
  Simba SC, mabingwa wa Tanzania Bara leo walitengeneza nafasi zaidi ya tatu nzuri, lakini bahati mbaya umaliziaji ukawanyima japo bao moja katika mchezo huo mzuri. 
  Kiungo Mnyarwanda wa Simba SC, Haruna Niyonzima akiondoka na mpira mbele ya mchezaji wa Big Bullets leo  
  Kiungo Hassan Dilunga akituliza mpira kwa ustadi mkubwa leo Uwanja wa Taifa 
  Mshambuliaji Mohammed Rashid akimpita beki wa Big Bullets, anayejaribu kuutelezea mpira

  Kikosi cha Big Bullets kilichotoa sare ya bila kufungana na Simba SC leo  

  Kikosi cha Simba SC kilichomenyana na Big Bullets ya Malawi leo

  Alianza mlinzi wa kati, Yussuf Mlipili dakika ya 10 alishindwa kutumia vema nafasi nzuri aliyotengenezewa na mshambuliaji Mohamed Rashid kwa kupiga shuti lililotoka nje setimeta chache, kabla ya kiungo Muzamil Yassin naye kupiga shuti la umbali wa kita 23 likapaa juu ya lango.
  Naye Nahodha wa leo, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ akaikosesha Simba SC bao la wazi zaidi akiwa amebaki yeye na kipa wa Big Bullets, Enerst Kakhombwe akapiga nje na kuwaacha mashabiki ‘wakitapika’. 
  Mtokea benchi, beki Muivory Coast, Serge Wawa Pascal naye akamjaribu kipa wa Bullets, Kakhombwe dakika ya 84 kwa shuti kali, ambalo mlinda mlango huyo alilidaka kiulaini.
  Bullets nao walilitia misukosuko lango la Simba SC ambalo leo lilikuwa linalindwa na Deogratius Munishi ‘Dida’ mara mbili dakika ya nne akidaka mpira wa kichwa uliopigwa na kiungo wa Henry Kabichi na dakika ya 88 shuti la Righteous Banda lilipaaa juu kabisa.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa: Deogratias Munishi ‘Dida’, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Yussuf Mlipili, James Kotei, Paul Bukaba, Said Ndemla/Serge Wawa dk46, Muzamil Yassin, Hassan Dilunga, Mohamed Rashid/Nicholas Gyan dk46, Haruna Niyonzima/Marcel Kaheza dk83 na Mohammed ‘Mo’ Ibrahim/Rashid Juma dk46.
  Big Bullets: Enerst Kakhombwe, Piliran Zonda, Emmanuel Zoya, Miracle Gabeya, Sankhani Mkandawire, Bashir Maunde, Henry Kabichi, Nelson Kangunje/Ernest Petro dk79, Righteous Banda/Dalitso Sailes dk75, Mcfapqlen Mgwira na Bright Munthali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAONYESHA NI TISHIO, YATOA SARE NA BIG BULLETS LICHA YA KUWAKOSA NYOTA WAKE KIBAO WA KIKOSI CHA KWANZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top