• HABARI MPYA

    Thursday, November 22, 2018

    AZAM FC YAICHAPA RUVU SHOOTING 2-1 CHAMAZI NA KUZIDI KUPAA KILELENI MWA LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanya kweli baada ya kuinyuka mabao 2-1 Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliomalizika kwenye Uwanja wa Azam Complex leo Alhamisi usiku.
    Ushindi huo unaihakikishia Azam FC nafasi ya kuendelea kubakia kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha pointi 33 baada ya kushinda mechi tatu na sare tatu ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja.
    Azam FC ilionekana kucheza vema kwenye mchezo huo hasa dakika 25 za mwanzo za kipindi cha kwanza na kufanikiwa kupata bao la uongozi dakika ya 11 lililofungwa na winga Ramadhan Singano ‘Messi’, akimalizia kazi nzuri ya Tafadzwa Kutinyu.
    Hilo linakuwa bao la kwanza kwa Singano msimu huu, kwa kiasi kikubwa akionekana kuwa na kiwango kizuri hali iliyomfanya Kocha Mkuu, Hans Van Der Pluijm, kumuamini mara kwa mara kwa kumuanzisha kwenye mechi kikosini.
    Dakika 16 baadaye, Said Dilunga, aliisawazishia Ruvu Shooting akitumia makosa yaliyofanywa kwenye eneo la ulinzi la Azam FC, na bao hilo kufanya kipindi cha kwanza kimalizike kwa timu zote kuwa nguvu sawa.
    Matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex waliingia kipindi cha pili kwa kasi wakitaka kupata bao la ushindi, lakini umakini kwenye eneo la ushambuliaji uliweza kuikosesha mabao.
    Kiungo mshambuliaji, Kutinyu ambaye alionekana kuwa kwenye kiwango bora kwenye mchezo huo, aliipatia bao la pili Azam FC baada ya kupokea pasi ya Bruce Kangwa na kupiga shuti lililobabatiza mabeki na mpira kujaa wavuni.
    Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitapumzika kwa siku tatu kabla ya kuanza mazoezi Jumatatu kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Stand United utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Desemba 4, mwaka huu saa 1.00 usiku.
    Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Razak Abalora, Abdallah Kheri, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C), Mudathir Yahya, Joseph Mahundi, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Danny Lyanga/Yahya Zayd dk 62, Tafadzwa Kutinyu, Ramadhan Singano/Mbaraka Yusuph dk 78
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAICHAPA RUVU SHOOTING 2-1 CHAMAZI NA KUZIDI KUPAA KILELENI MWA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top