• HABARI MPYA

    Friday, April 17, 2015

    HATUJUI LOLOTE KUHUSU YANGA, TUTAINGIA KICHWA KICHWA- BENZARTI

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    KIKOSI cha Etoile du Sahel ya Tunisa kimefanya mazoezi ya kuujaribu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya mechi yao na Yanga kesho, lakini kocha Faouzi Benzarti amesema hajui lolote kuhusu wapinzani wao hao.
    Kanuni za mashindano yote ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zinaagiza timu mgeni kufanya mazoezi katika Uwanja wa mechi siku moja kabla na Etoile wametumia fursa hiyo leo.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mara baada ya mazoezi yao, Benzarti amesema kutokana na ufinyu wa muda hawakufanikiwa kuwafanyia upelelezi wa kutosha Yanga lakini watajaribu kupambana nao wakitumia uzoefu zaidi.
    Benzarti amesema hakuna kipya katika mchezo wa soka na kwamba Etoile haiwezi kuwaogopa Yanga, lakini amewataka wachezaji wake kuwa makini kutokana na kutofanya utafiti wa kutosha.
    Wachezaji wa Etoile du Sahel wakimsikiliza kocha wao kabla ya kuanza mazoezi
    Wachezaji wa Etoile wakifanya mazoezi meopesi
    Wachezaji wa Etoile wakiwa mazoezini Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo



    "Hakuna kitu kipya sana katika soka, nataka tukapambane, hii ni mechi muhimu, hatuwajui Yanga kwa kuwa tangu tulipomaliza mechi yetu hatukupata muda wa kutosha kutafuta taarifa zao kama tulivyokuwa tunataka,"alisema Bunzarti.
    Etoile walifanya mazoezi mepesi ya kuondoa uchovu wa saa tisa safarini, lakini kivutio kilikuwa ni baadhi ya wachezaji wakigombea kunywa maji mara kwa mara wakilalamika hali ya joto la hapa nchini.
    Yanga wanamenyana na Etoile kesho katika Raundi ya Pili ya Kombe la Shirikisho Afrika, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Etoile du Sahel wametua Saa 10:10 Alfajiri ya leo kwa Ndege ya kukodi ya kampuni ya Nouvelair bj 4870 wakiwa na msafara wa watu 56 kwa ajili ya mchezo huo wa kwanza hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika.
    Msafara wao umeongozwa na Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tunisia (FTF), Krifa Jalel na wamekuja pia na Rais wa klabu yao, Charefeddine Ridha, wachezaji 19, benchi la ufundi lenye watu 13, Waandishi wa Habari 12 na wapenzi 10.
    Baada ya kutoka ndani ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Etoile du Sahel waliopokewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro, walielekea katika hoteli ya Ledger Plaza zamani Bahari Beach eneo la Kunduchi.
    Mchezo huo, utachezeshwa na marefa kutoka Msumbiji Samuel Chirindiza, Arsenio Marenguka, Celio de Jesus Musabe, Jose Maria Bachide na Kamisaa Salah Ahmed Mohamed kutoka Sudan.
    Wakati ESS iliyoanzia Raundi ya Kwanza ambako iliitoa Benfica ya Luanda kwa jumla ya mabao 2-1, ikishinda 1-0 kwao na kulazimisha sare ya 1-1 Angola, Yanga ilizitoa BDF ya Botswana kwa jumla ya mabao 3-2 katika Raundi ya Awali na FC Platinum ya Zimbabwe kwa jumla ya mabao 5-2 katika Raundi ya Kwanza.
    Yanga SC tangu imalize mchezo wake wa Ligi Kuu na Mbeya City Jumamosi ambao ilishinda 3-1, imekuwa kambini katika hoteli ya Tansoma, eneo la Gerezani, ikifanya mazoezi Uwanja wa Karume na Taifa kujiandaa na mechi hiyo ya kesho. 
    Viingilio katika mchezo huo vitakuwa ni Sh. 5,000 kwa majukwaa yenye viti vya rangi ya bluu na kijani, Sh. 10,000 kwa viti ya Rangi ya Chungwa, Sh. 20,000 VIP C, Sh. 30,000 VIP B na Sh. 40,000 VIP A.
    Tiketi zinapatikana tangu asubuhi leo Uwanja wa Karume, Billicanas, Feri, Dar Live, Buguruni Sheli, Ubungo Stendi ya mabasi, Uwanja w Taifa, makao makuu ya Yanga makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani na Mwembe Yanga, Tandika. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HATUJUI LOLOTE KUHUSU YANGA, TUTAINGIA KICHWA KICHWA- BENZARTI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top