• HABARI MPYA

    Wednesday, April 15, 2015

    BURIANI MCHA KHAMIS, ‘STRAIKA’ WA KUKUMBUKWA ZANZIBAR

    Mcha Khamis enzi za uhai wake
    Na Hafidh Abdulhabib, ZANZIBAR
    MIEZI kumi ikiwa imepita tangu klabu ya KMKM ya Zanzibar kufiwa na aliyekuwa nahodha wake mstaafu marehemu Ali Issa Simai ‘Kepteni’, mshambuliaji mwengine wa zamani wa mabaharia hao Mcha Khamis Mcha amefariki dunia usiku wa jana.
    Taarifa zilizopatikana kutoka kwa waliokuwa wachezaji wenzake wastaafu, zimefahamisha kuwa, Mcha ambaye ni baba mzazi wa kiungo mahiri wa Azam FC ya Dar es Salaam, Khamis Mcha ‘Viali’, alikuwa amelazwa hospitali ya taifa Muhimbili akitibiwa maradhi ya kibofu cha mkojo.
    Mshambuliaji huyo aliyefariki akiwa na umri wa miaka 60, atakumbukwa kwa mchango wake  mkubwa alioutoa kwa timu ya KMKM tangu ikiitwa Navy, na pia timu za taifa za Zanzibar na Tanzania katika vipindi tofauti.
    Abdalla Maulid, beki wa zamani wa KMKM na rafiki wa karibu wa marehemu, alimsifia Mcha kutokana na uwezo aliokuwa nao katika kuzifumania nyavu hata katika mazingira magumu.

    .

    Sentahafu wa zamani wa KMKM ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa jimbo la Jang’ombe (CCM) Mohammed Rajab, akiwaongoza wananchi na wapenda michezo wa mjini Zanzibar, kuupokea mwili wa marehemu Mcha Khamis, mchezaji wa zamani wa KMKM na Zanzibar Heroes marehemu Mcha Khamis, aliyefariki dunia usiku wa jana hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam. 
    (Picha na Zanzinews Blog).

    Aidha alisema marehemu alikuwa na kasi kubwa iliyowapa shida mabeki waliokuwa wakimchunga kila aliposhuka dimbani.
    Kihistoria, Mcha aliyemudu kuchezea nafas za winga wa kushoto na kulia, na kiungo mshambuliaji, alijiunga na Navy (sasa KMKM) mwaka 1975 akianzia kikosi cha pili hadi mwaka 1977 alipopandishwa timu ya kwanza.
    Kutokana na kiwango chake kizuri, mwaka 1978, alichaguliwa katika timu ya Taifa ya vijana ya Zanzibar kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Chalenji ya vijana yaliyokuwa yafanyike nchini Somalia, lakini haikwenda kutokana na mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu hapa nchini.
    Mwaka 1982 aliitwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) na kuichezea dhidi ya Uganda kuwania kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika iliyokuwa ikichezwa kwa mtoano, lakini ikatolewa.
    Pamoja na kuibeba vyema klabu yake katika ligi kuu ya muungano kuanzia mwaka 1976 na kufanikiwa kutwaa ubingwa mwaka 1984, marehemu pia aliisaidia Navy (sasa KMKM) kucheza klabu bingwa Afrika mwaka 1978, ambapo walifika hatua ya nne bora.
    Pia mwaka 1978 alikuwemo katika timu ya Taifa ya Zanzibar hadi 1987.
    Marehemu alikuwa kati ya wachezaji wa Navy waliofundishwa kwa vipindi tofauti na makocha wa kigeni, Edmund Hensen kutoka Ujerumani, Dick Rooks na Erick Wistenly wa Uingereza, pamoja na kocha mzalendo marehemu Mzee Kheri.
    Aidha miongoni mwa mafanikio mengine ya kujivunia kwa mwanandinga huyo mstaafu, ni kuisaidia Navy kutinga hatua ya nane bora kwenye michuano ya Kombe la Washindi Afrika, na baadae kuipa ubingwa wa Muungano mwaka 1984.
    Mwaka 1986 aliijunga na klabu kongwe ya Miembeni SC na kuisaidia kutwaa ubingwa wa Zanzibar msimu wa 1987 na kuichezea timu hiyo hadi mwaka 1988.
    Baada ya kustaafu soka, marehemu akawa anajumuika na wakongwe wenzake katika timu ya Zanzibar Veterans, ambayo aliichezea kwa mara ya mwisho Agosti 4, 2013 katika mechi iliyobeba ujumbe wa kumaliza malaria nchini chini ya Mfuko wa Rais wa 42 wa Marekani, Bill Clinton aliyekuwa ziarani hapa nchini.
    Mazishi yake yamefanyika alasiri ya leo kijijini kwao Mkwajuni Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja na kuhudhuriwa na wananchi na wanamichezo wengi.
    Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema Peponi. Amin
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BURIANI MCHA KHAMIS, ‘STRAIKA’ WA KUKUMBUKWA ZANZIBAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top