• HABARI MPYA

  Thursday, December 04, 2014

  YANGA SC: HATUTARUDIA MAKOSA NANI MTANI JEMBE 2

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imesema kwamba haitarejea makosa tena katika mchezo ujao wa Nani Mtani Jembe 2, Jumamosi wiki ijayo watakapokutana na mahasimu wao, Simba SC.
  Meneja Masoko wa Yanga SC, George Simba amesema leo katika Mkutano na Waandishi wa Habari mjini Dar es Salaam kwamba, wamejipanga kulipa kisasi cha kufungwa 3-1 mwaka jana.
  “Sisi tumejiandaa vizuri ili kulipa kisasi katika mchezo huo. Hatutakuwa tayari kurudia makosa tuliyoyafanya mwaka jana, tunawaomba wapenzi wetu wajitokeze kwa wingi siku hiyo kushuhudia burudani,”amesema Simba.
  Kuhusu maandalizi ya timu, Simba amesema kwamba kikosi cha Yanga SC kitaingia kambini mapema wiki ijayo na kwamba hawana majeruhi hata mmoja hadi sasa.
  Nani Mtani Jembe 2 inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itachezwa Jumamosi, Desemba 13, 2014 kuanzia Saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  George Simba kushoto amesema Yanga SC hawatarudia makosa Nani Mtani Jembe 2

  Pambano hili ni hitimisho la kampeni ya NMJ iliyoendeshwa kwa wiki 10 ikiwapa fursa mashabiki wa timu hizi kuchangia timu zao kwa kunywa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, wadhamini wa klabu hizo.
  Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace Wambura ametaja viingilio vya mechi hiyo kuwa ni shilingi 30,000 kwa VIP B, 20,000/= VIP C, 15,000/= kwa viti vya rangi ya chungwa kiingilio kitakuwa ni sh 15,000 huku viti vya bluu na kijani tiketi zikiuzwa kwa sh. 7,000/=.  
  Wambura amesema pambano hilo litakalosimamiwa na TFF litaanza Saa 10:00 jioni na litachezwa kwa dakika 90 tu ambapo kama muda timu hizo hazitafungana basi mikwaju ya penati itapigwa ili mshindi apatikane. 
  Taji la Nani Mtani Jembe linashikiliwa na Simba ambao waliwafunga mahasimu wao 3-1 katika mechi iliyochezwa Disemba 21, 2013. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC: HATUTARUDIA MAKOSA NANI MTANI JEMBE 2 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top