• HABARI MPYA

  Monday, December 08, 2014

  UKIMNUNUA MSANII WA DANSI KWA MILIONI 15 KIPINDI HIKI NI LAZIMA UKAPIMWE AKILI

  Unapoona Cristiano Ronaldo ananunuliwa na Real Madrid kwa pauni milioni 80 kutoka Manchester United, unapigwa na butwaa.
  Lakini siku chache baada ya utambulisho wake kwenye klabu yake mpya, unasoma namna mamilioni ya jezi zenye jina lake zinavyonunuliwa kama njugu, unafarijika kidogo kwamba angalau anaanza kurudisha pesa kwa mlango mwingine.
  Na baadae unapoona mipira anayodumbukiza wavuni, mataji anayochangia, ukichanganya na mshiko wa mauzo ya tiketi katika kila mechi, pesa kedekede za wadhamini, unakubali kuwa jamaa hawakuwa wendawazimu kumnunua kwa mamilioni ya pesa.

  Kwa bahati mbaya sana Watanzania tumekuwa tukiiga mambo mengi bila kujali mazingira yaliyotuzunguka, ukiangalia namna timu zetu zinavyonunua wachezaji bila kujali vyanzo vyao vya pesa, utagundua kuwa wazimu wa kuiga umetupanda kichwani.
  Hali hiyo haikomei kwenye soka tu, kituko zaidi ni kwenye muziki wa dansi wa Tanzania na hapo ndipo utakoma ubishi - Wanamuziki wananunuliwa kwa bei za ajabu, mikataba minono inayoandamana na misharaha mikubwa, lakini wanachokwenda kukiingiza hakifidii hata robo ya pesa zilizomwagwa kwaajili yao.
  Unamunua msanii ambaye licha ya umaarufu wake aliotengenezewa na bendi yake ya zamani, lakini bado hana uwezo wa kuhama na mashabiki japo 80, unamtambulisha leo ukitaraji kuwa kuanzia kesho utaongeza angalau watu 200 kwenye maonyesho ya bendi yako, mwisho wa siku unagundua wameongezeka 20 tu.
  Unajipa moyo kuwa labda mambo yatabadilika, siku zinakwenda, miaka inaondoka hali ni ile ile, msanii anamaliza mkataba wake mara huyoo anatimka anarudi bendi yake ya zamani ‘kubust’ jina lake lililofifia.
  Hata kama utasingizia kuwa pesa zimetolewa na waketereketwa wa bendi, lakini ni ukweli usiopingika kuwa soko la muziki wa dansi kwa sasa haliruhusu kumnunua msanii kwa bei ya ‘kufuru’.
  Nimewahi kusema mara kadhaa huko nyuma kuwa soko la muziki wa dansi lipo kwenye kipindi cha mpito, kipindi cha kupambana na ‘umauti’. Kwanini nasema dansi lipo kwenye kipindi cha mpito? Nitataja sababu kadhaa.
  Moja: (Hii nilishawahi kuisema huko nyuma) soko la nyimbo za dansi ni kama limekufa, wasambazaji hawanunui muziki dansi, mauzo ya audio CD na DVD za dansi ni sawa na sifuri, hata makampuni ya miito ya simu (Ring tone) hayana ‘time’ na muziki wa dansi.
  Pili: Wahudhuriaji wa maonyesho ya dansi wameyeyuka, asilimia 90 ya bendi zote hazifikishi mahudhurio ya watu 300 katika kila onyesho iwe ni kwa kiingilo au kiingilio kinywaji.
  Tatu: Mfumuko wa maonyesho ya kiingilio kinywaji chako, umerejea kwa kasi kubwa na kuzidi kuporomosha soko la muziki wa dansi  - sasa hivi sio ajabu kukuta bendi moja inapiga kwa kiingilio huku bar tatu za jirani zinapiga dansi bure, ukitajiwa pesa zinazopewa bendi kwa show hizo za bure, utatingisha kichwa kwa masikitiko, kama ipo inayopewa milioni 1 basi   ni ya kutafuta kwa tochi.
  Nne:  Vyombo vya habari vimeutosa muziki wa dansi, si radio, televisheni wala magazeti, kila kukicha yanatoka masharti ya ajabu, yakiwemo ya kupunguza urefu wa nyimbo, lakini hata masharti hayo yanapofanyiwa kazi, bado vyombo vya vingi vya habari vinaendelea kuufungia vioo muziki wa dansi.
  Tano: Wadhamini wameutupa mkono muziki wa dansi, hakuna kampuni inayotaka kuwekeza kwenye dansi, ukichunguza sababu wala hutawalaumu … ni media inawalazimisha kufanya hivyo, utawekaje pesa zako katika muziki ambao haukubaliki kwenye vyombo vya habari?
  Ni kwa hali kama hiyo ndipo nalazimika kusema kuwa anayemnunua mwanamuziki wa dansi kwa milioni 15, anastahili kupimwa akili – Unampa msanii mpya milioni 10 na upuuzi huku baadhi ya wasanii wako wa zamani wanasubiri hadi tarehe 50 kupata angalau nusu ya mishahara wao, kama si wazimu ni nini? KAPIMWE.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: UKIMNUNUA MSANII WA DANSI KWA MILIONI 15 KIPINDI HIKI NI LAZIMA UKAPIMWE AKILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top