• HABARI MPYA

  Sunday, December 14, 2014

  MASHABIKI SIMBA SC WANA HAMU NA UBINGWA TENA, AVEVA ANALIJUA HILO?

  SIMBA SC imeshinda mechi ya pili ya mashindano chini ya Rais Evans Aveva na kocha Mzambia Patrick Phiri, baada ya jana kuifunga Yanga SC mabao 2-0.
  Awali, zaidi ya mechi za kirafiki Simba SC ilishinda mechi moja ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting ya Pwani, nyingine sita ikitoa sare zote.
   Ushindi wa jana ni katika mechi ya Nani Mtani Jembe Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, shukrani kwao kiungo Awadh Juma na mshambuliaji Elias Maguri, waliofunga mabao hayo.
  Awadh Juma alifunga bao la kwanza baada ya kukutana na mpira uliookolewa na kipa Deo Munishi 'Dida' kufuatia mpira wa adhabu uliopigwa na Emmanuel Okwi dakika ya 30, umbali wa mita 23.

  Elias Maguri aliifungia Simba SC bao la pili dakika ya 42 akimalizia mpira uliorudi baada ya kugonga mwamba kufuatia yeye mwenyewe kupiga kichwa akiunganisha mpira wa kurushwa kutoka wingi kulia.
  Simba SC walistahili ushindi jana, kwa sababu walicheza vizuri na kuwazidi wapinzani wao, walio chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo.
  Desemba mwaka jana, Simba SC ikiwa chini ya Rais, Alhaj Ismail Aden Rage na Kocha Mcroatia, Zdravko Logarusic iliwafunga tena Yanga SC katika Mtani Jembe mabao 3-1.
  Lakini Wekundu wa Msimbazi waliporudi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara hawakuwa na matokeo mazuri sana na wakamaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo.
  Ukawa mwaka wa pili mfululizo, Simba SC siyo tu inakosa ubingwa, bali hata nafasi ya kucheza michuano ya Afrika, mara zote wakizidiwa na Azam FC na Yanga SC.
  Mashabiki wa Simba SC wana kiu ya kuiona tena timu yao ikicheza michuano ya Afrika, baada ya kuikosa kwa miaka miwili iliyopita.
  Mashabiki wa Simba SC wana hamu ya kuiona timu yao ikiinua tena taji la ubingwa wa Ligi Kuu, baada ya kulikosa kwa miaka miwili iliyopita.
  Mashabiki wa Simba SC kwa sasa hawana wasiwasi na mechi dhidi ya Yanga SC, wanaamini kabisa viongozi wao wanaweza kuicheza na kushinda.
  Lakini bado wanasubiri kuona tena Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu linapelekwa Mtaa wa Msimbazi kwa maandamano ya nderemo, hoi hoi na vifijo.
  Na kuona pia kikosi cha timu kinasafiri kwenda kucheza michuano ya Afrika, badala ya mechi za kirafiki dhidi ya timu za Uganda na Kenya mara kwa mara.
  Baada ya ushindi wa jana, viongozi wa Simba SC, makocha na wachezaji waliungana na mashabiki wao kusherehekea kuendeleza ubabe kwa mahasimu, Yanga SC.
  Kama mwaka jana tu, Simba SC walifurahia sana ushindi wa Nani Mtani Jembe wakasahu kujipanga vyema kwa ajili ya Ligi Kuu, matokeo yake hata Mbeya City wakawa bora zaidi yao.
  Simba SC hawakuwa na timu mbovu msimu uliopita, ndiyo maana waliifunga 3-1 Yanga SC- na hata msimu huu, wana timu nzuri ambayo jana imewalaza 2-0 mahasimu.
  Kikubwa ambacho Simba SC, kuanzia viongozi, wachezaji na makocha wanatakiwa kufanya kwa sasa ni kuelekeza nguvu zao katika Ligi Kuu.
  Simba SC hawatakiwi kubweteka baada ya ushindi wa bonanza la Nani Mtani Jembe jana, kwani kufanya hivyo haitakuwa ajabu na msimu huu pia wakawa nje ya timu mbili za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
  Wakati nawapongeza Simba SC kwa ushindi wa bonanza au fete fete kama asemavyo Mwenyekiti wa Yanga SC, Yussuf Manji jana, nawakumbusha tu; Mashabiki wao wana hamu na ubingwa tena. Alamsiki. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MASHABIKI SIMBA SC WANA HAMU NA UBINGWA TENA, AVEVA ANALIJUA HILO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top