• HABARI MPYA

  Wednesday, December 10, 2014

  FID-Q AZINDUA KAMPENI YA KUHAMASISHA VIJANA KUSHIRIKI KATIKA MCHAKATO WA UCHAGUZI WA VIONGOZI WA TAIFA LETU.

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSANII nguli wa miondoko ya Hip-hop Fareed Kubanda - Fid Q amekutana na waandishi wa habari katika ukumbi wa Sports Lounge katikakati ya jiji la Dar es Salaam, kujadili maswala ya msingi yenye mustakabali chanya kwa maendelo ya taifa hili. Ameitisha mkutano huu akiwa kama kijana na mwenye nafasi na ushawishi kwa vijana wenzie katika ushiriki wa kuleta mabadiliko chanya na maendeleo ya nchi yetu.
  Fid Q amesukumwa kuzungumza na waandishi wa habari baada ya kutanabai kwamba vijana japo ni asilimia 80 ya taifa lakini hawana mwamko na msukumo wa kujitokeza kushiriki mchakato wa uchaguzi wa viongozi waowataka na wanaowaamini wanauwezo wa kuleta mabadiliko ya ki nidhamu kwenye masuala ya msingi ya taifa letu.
  Fid Q katikati akizungumza na Waandishi wa Habari. kulia ni Dito na kushoto Said Fela
  Kutoka kulia Babu Tale, Dito, Fid, Fela na Lamar.

  “Kuna kitu kimoja ambacho watu wengi hasa hasa vijana wenzangu hawakifahamu, Nchi  yetu ni changa sana. Vijana nchi hii chini ya umri wa miaka 35 ni zaidi ya asilimia 80 ya idadi ya watu, wakati watu wazima zaidi ya miaka 60 ni asilimia chini ya 5 ya watanzania wote. Hizi ni takwimu za sensa iliyopita.  Nimetanguliza takwimu mapema kwa sababu, twakimu huwa hazisemi uwongo. Changamoto zinalolikumba taifa hili kwa kiasi kikubwa zinatuathiri sisi vijana wa nchi hii ambao ndio wengi wetu. Madhara yanayotokana na uongozi mbovu, vile vile yanatuathiri sana sisi vijana kwa wingi wetu. Tutake tusitake, ustawi na kunawiri kwa vijana ndio kutaamua mustakabali wa Tanzania, vijana tukilala basi na Tanzania pia italala.”  Alisema Fid Q.
  Bado kuna changamoto ya upatikanaji wa ajira kwa vijana. Vijana wengi wamezagaa mitaani bila shughuli za kufanya. Hata wale wenye degree hawana kazi. Vijana wanakata tama na kuona kwamba wao sio sehemu ya taifa hili. Kuna changamoto ya viongozi waadilifu watakaosimamia kuhakikisha kwamba keki ya taifa inagawanywa kwa Watanzania wote na hailiwi na wachache.
  Baada ya utangulizi huo, ni dhahiri kwamba kwenye uchaguzi huu wa serikali za mitaa unaoendelea, na uchaguzi mkuu wa 2015 lazima vijana tuamke na tushiriki kikamilifu. Kwanza, vijana wenye uwezo na sifa za kugombea nafasi za uongozi ni lazima wafanye hivyo, pili vijana wenye vigezo vya kupiga kura pia ni lazima wafanye hivyo maana ni wajibu wetu, tatu, vijana ni lazima tushiriki kikamilifu katika mchakato wa kampeni ili kuhakikisha ishu zetu za msingi zinajadiliwa na wagombea na zinapewa kipaumbele. 
  Kama vijana wanakuwa na hofu basi niwakumbushe kwamba, Mwalimu Nyerere alikabidhiwa nchi hii akiwa na miaka 39 tu na kuanza harakati za kupigania Uhuru ambao tumeuenzi jana. Alikuwa ni kijana mdogo tu. Mzee wetu Dr. Salim Ahmed Salim alianza kuwa mwanadiplomasia mahiri akiwa na rika dogo tu, akiwa na umri wa miaka 22  alikuwa Balozi wa Tanzania, nchini Misri. Mifano ipo mingi, hivyo vijana tusipate woga - Tumechangia kupatikana kwa Uhuru na kujenga nchi hii, na sasa ni wakati mwingine tena wa kuibadilisha nchi yetu.
  “Hivyo mimi Fareed Kubanda, nimeamua kufanya matamasha ili kusimamia haya niliyoyasema hapo juu. Kwa kutumia nafasi zenu ndugu wana habari naomba mnisaidie kutangaza azma yangu hii pamoja na nitawapigia baadhi ya wasanii wenzangu kuwaomba waniunge mkono ili tufanikishe hili na tushiriki katika kuleta uongozi utako leta mabadiliko tunayoyataka na kwa kasi yetu sisi vijana.”
  Fid Q aliendelea “Ninatumaini kwamba wasanii wenzangu wataniunga mkono, ili kuanza kuwaamsha vijana wenzetu, tuweze kutimiza wajibu wetu wa kihistoria wa kufanya mabadiliko katika nchi yetu, hasa pale tunapokuwa tunahitajika sana na jamii. Tayari nimefanya mazungumzo na Mkubwa Fela, Babu Tale, Mwana FA, Nick wa Pili, Lamar, P-Funk, Mwasiti, Barnaba, Ditto ambao wamekubali kuwa sehemu ya harakati hizi. Bado nahitaji wasanii wengine wengi washiriki ki mawazao, hali na mali kufikia lengo kuu la Tanzania mpya na bora zaidi”.
  Huu ni mwanzo wa harakati hizi, mwakani tutafanya amsha amsha kubwa ya vijana. Mwaka huu tunasema Tuonane January (#Tuo8January). Tutengeneze nchi yetu!! Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania!
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: FID-Q AZINDUA KAMPENI YA KUHAMASISHA VIJANA KUSHIRIKI KATIKA MCHAKATO WA UCHAGUZI WA VIONGOZI WA TAIFA LETU. Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top