• HABARI MPYA

  Tuesday, October 22, 2013

  REFA WA DODOMA APEWA MECHI YA SIMBA NA COASTAL, YANGA NA RHINO KAZI IPO TAIFA KESHO

  Na Boniface Wambura, Ilala
  LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara  inaendelea kesho (Oktoba 23 mwaka huu) kwa mechi tatu; ambapo Yanga itaikaribisha Rhino Rangers katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Coastal Union inaikaribisha Simba katika mechi itakayopigwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga na kuchezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana kutoka Dodoma.
  Tanzania Prisons ambayo imepoteza mechi mbili zilizopita ugenini dhidi ya Ashanti United na Simba inarejea uwanja wake wa Kumbukumbu ya Sokoine kwa kuikaribisha Kagera Sugar.
  Simba SC

  Nayo Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inaendelea kesho (Oktoba 23 mwaka huu) kwa mechi moja ya kundi A itakayozikutanisha Tessema na Villa Squad kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.
  Wakati huo huo: Uchaguzi wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPL Board) utafanyika Oktoba 25 mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Golden Jubilee Tower.
  Kwa mujibu wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wajumbe wanaounda Mkutano wa Uchaguzi ni wenyeviti kutoka klabu 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), na 14 wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).
  Wagombea kwenye uchaguzi huo ni Hamad Yahya Juma (Mwenyekiti), Said Muhammad Said Abeid (Makamu Mwenyekiti) wakati wanaoumba ujumbe wa Kamati ya Uendeshaji ni Khatib Omari Mwindadi na Kazimoto Muzo.
  Katika hatua nyingine, TFF imepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mjumbe wa Bodi ya klabu ya Ashanti United, Jimmy Mhango kilichotokea jana (Oktoba 21 mwaka huu).
  Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani Mhango aliutumikia mpira wa miguu kwa muda mrefu, tangu akiwa mchezaji, kocha na baadaye kiongozi.
  Kabla ya kuingia kwenye Bodi ya Ashanti United, enzi za uchezaji wake alichezea timu za Mapinduzi ya Dodoma, Ushirika ya Moshi na Pan African ya Dar es Salaam. Pia aliwahi kuwa Kocha Mkuu wa Ashanti United.
  TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Mhango, klabu ya Ashanti United na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
  Maziko yamefanyika leo mchana katika makaburi ya Abeid (Mchikichini) Dar es Salaam. Mungu aiweke roho ya marehemu Mhango mahali pema peponi. Amina
  Naye Makamu wa Pili wa Rais wa TFF, Ramadhan Nassib ametoa sh. milioni moja kwa waamuzi waliochezesha mechi ya Simba na Yanga iliyochezwa wikiendi iliyopita jijini Dar es Salaam.
  Nassib ambaye alichaguliwa katika nafasi hiyo akiwakilisha klabu amesema ametoa fedha hizo ili kuwapongeza waamuzi hao kwa kuchezesha vizuri mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya mabao 3-3.
  “Waamuzi wanapofanya vibaya tunawaadhibu, hivyo wakifanya vizuri wanastahili kupongezwa pia. Vilevile kuwapongeza ni kuwaongezea ari ya kuchezesha vizuri zaidi,” amesema.
  Israel Nkongo ndiye aliyeongoza jopo hilo ambapo mwamuzi msaidizi namba moja alikuwa Hamis Chang’walu wakati namba mbili alikuwa Ferdinand Chacha. Mwamuzi wa mezani alikuwa Oden Mbaga.
  Waamuzi wote hao wana beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), na watoka Dar es Salaam ukiondoa Chacha ambaye maskani yake ni Bukoba mkoani Kagera.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: REFA WA DODOMA APEWA MECHI YA SIMBA NA COASTAL, YANGA NA RHINO KAZI IPO TAIFA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top