• HABARI MPYA

  Tuesday, October 29, 2013

  YANGA SC YAUA 3-0 MGAMBO JKT WALIOFUNGWA 7-0 NA SIMBA LIGI KUU

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  YANGA SC imeendelea vyema na jitihada za kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya leo kuifunga Mgambo JKT mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.  
  Ushindi huo dhidi ya Mgambo iliyofungwa 7-0 na Simba SC, unaifanya Yanga SC itimize pointi 22, baada ya kucheza mechi 11, Azam FC inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 23 sawa na Mbeya City. 
  Hadi mapumziko, tayari Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na beki wa kimataifa wa Rwanda, mwenye asili ya DRC, Mbuyu Twite dakika ya 32.
  Didier Kavumbangu akishangilia baada ya kufunga bao la tatu

  Twite alifunga bao hilo kwa shuti la mbali baada ya kuanzishiwa mpira wa karibu wa adhabu na kiungo Athumani Iddi ‘Chuji’.
  Yanga ilitawala zaidi mchezo kipindi hicho na kukosa mabao ya wazi zaidi ya matatu, lakini Mgambo nayo ilitengeneza nafasi mbili nzuri za kufunga ikashindwa kuzitumia.
  Kipindi cha pili, Yanga tena walirudi na moto na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 50, mfungaji Hamisi Kiiza kwa penalti, baada ya kipa Tony Kavishe kumchezea rafu mshambuliaji Didier Kavumbangu kwenye eneo la hatari. 
  Bao hilo liliwachagiza Yanga na kuendelea kushambulia kwa kasi lango la timu hiyo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na hatimaye kufanikiwa kupata bao la tatu dakika ya 67, mfungaji Kavumbangu.
  Kavumbangu alifunga bao hilo akiunganisha krosi maridadi ya Simon Msuva, aliyeanzishiwa mpira wa kurusha wa karibu na Mrisho Ngassa.  
  Baada ya bao hilo la tatu, Yanga SC walionekana kuridhika na kuanza kucheza mchezo wao wa kuremba, pasi nyingi na madoido na Mgambo walijaribu kutaka kutumia mwanya huo kupata japo bao la kufuti machozi, lakini kipa Deo Munishi ‘Dida’ alikamilisha dakika 180 bila nyavu zake kuguswa tangu aanze kudaka msimu huu akimpokea Ally Mustafa ‘Barthez’. 
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Rajab Zahir/Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva/Reliants Lusajo, Frank Domayo, Didier Kavumbangu, Mrisho Ngassa/Jerry Tegete na Hamisi Kiiza.
  JKTMgambo; Tony Kavishe/Godson Mmasa, Daud Salum, Bashiri Chanache, George Akitanda, Bakari Mtama, Novat Lufunga, Malimi Busungu, Peter Mwalyanzi, Fully Maganga/Mohamed Samatta, Omar Yassin na Mohamed Nampoka/Nassor Gumbo.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YAUA 3-0 MGAMBO JKT WALIOFUNGWA 7-0 NA SIMBA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top