• HABARI MPYA

    Sunday, October 27, 2013

    TUCHAGULIENI WATU SAHIHI KWA MUSTAKABALI WA SOKA YETU

    UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) unafanyika leo katika ukumbi wa NSSF Water Front, Dar es Salaam na kwa mara ya kwanza baada ya miaka minane, bodi hiyo inatarajiwa kuwa na rais mpya.
    Beki wa kati wa zamani wa Pan Africans, Yanga na Nahodha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Leodegar Tenga hagombei tena baada ya kuongoza bodi hiyo kwa awamu mbili na sasa aliyekuwa Makamu wake wa kwanza katika awamu ya pili, Athumani Nyamlani anachuana na mpinzani wake (Tenga) katika uchaguzi uliopita, Jamal Malinzi kuwania kurithi kiti hicho.

    Nafasi inayoachwa wazi na Nyamlani inawaniwa kwa pamoja na Wallace Karia, Ramadhani Nassib na Imani Madega wakati pia watu kadhaa wamepitishwa kuwania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.
    Tenga jana amefungua Mkutano Mkuu wa TFF kwa kutoa nasaha zake, kukumbusha alipoikuta soka ya Tanzania na mabadiliko aliyoyafanya kwa ujumla na namna ambavyo amerudisha heshima katika mchezo huo nchini.   
    Tenga alielezea hayo kama mafanikio, kuvuta wawekezaji katika mchezo, kuondoa migogoro ndani ya soka yetu na timu ya taifa kushiriki CHAN mwaka 2009. 
    Pengine Watanzania walitaka zaidi ya hivyo ambavyo Tenga amethubutu kujivunia jana, katika miaka yake minane pale TFF zimepita fainali tano za AFCON na tatu za Kombe la Dunia, hatumo.
    Rwanda wamekuwa wenyeji wa fainali za vijana Afrika mara mbili, za U17 na U20 hatukwenda. Klabu zetu bado laini katika michuano ya Afrika- kwa ujumla kuna mambo ambayo unaweza kumpa heko Tenga, lakini vema akatambua kwamba anaondoka TFF kwa kiasi kikubwa akiwa hajawafurahisha Watanzania.
    Matarajio wakati anaingia madarakani yamekuwa tofauti na matokeo ya miaka yake nane pale Ilala. Hilo si kitu, siyo mwisho wa soka yetu bali ni mwisho wa utawala wa Tenga na ndiyo maana leo tuna uchaguzi mwingine Water Front.
    Kwa uzoefu, wapiga kura wa TFF huwa wanaingia kwenye Mkutano wa uchaguzi, wakiwa tayari wana maamuzi yao juu ya nani wanampigia kura, iwe kwa utashi au kushinikizwa na zaidi kwa kuhongwa.
    Siku hizi kuna hongo za aina yake- wagombea wanajipanga kwa muda mrefu kuelekea uchaguzi, kwa kuanzia kupachika watu wao kwenye vyama vya mikoa ili baadaye waende kuwapigia kura.
    Nitafafanua; mgombea Urais wa TFF alimuwezesha mtu akaenda kugombea uongozi wa mkoa na kushinda- sasa hapo maana yake anatengeneza mtandao wa kukusanya kura zake mapema.
    Tunasikia, kuna mgombea katika uchaguzi wa leo amefanikiwa kuweka watu wengi kiasi kwamba picha ya matokeo tayari imekwishaanza kuonekana. 
    Lakini pia Wajumbe wanahongwa moja kwa moja fedha na mara nyingi wagombea wanatapeliwa kwa kuliwa fedha zao na kuahidiwa kura, mwisho wa siku wanaanza kulalamika wameibiwa kura. Huna unachoweza kumuambia mpiga kura siku ya leo, tangu anapanda basi kutoka mkoani kwake, tayari anajua anakuja kufanya nini Dar es Salaam.
    Lakini vyema Wajumbe wakajua kwamba, ipo haja ya kumchagua mtu safi, ambaye ataivusha soka ya nchi hii katika anga nyingine. Tumesikia sera za wagombea, ingawa kwa wengine huwa na mapambio tu ya kampeni, lakini angalau hiyo inaweza kuwa dalili ya kwanza ya kumjua mtu safi kutokana na sera zake nzuri.
    Kama ana sera nzuri, akiwa pale Uwanja wa Karume hata kama atazembea kuzitekeleza, sisi tutamkumbusha sera zake na tutamrudishia vipeperushi vyake.
    Malinzi- Nyamlani ni kazi rahisi sana, kwa sababu watu hawa wawili wanajulikana vyema sasa katika soka ya nchi hii na rekodi zao zipo wazi, huwezi kupata tabu ya kuamua unamchagua nani. Lakini jambo moja tu, mchague mmoja kati yao, kwa sababu umejiridhisha huyu anaweza kuiletea mafanikio soka ya Tanzania. Uchaguzi mwema. Wikiendi njema. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TUCHAGULIENI WATU SAHIHI KWA MUSTAKABALI WA SOKA YETU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top