• HABARI MPYA

  Jumatano, Oktoba 30, 2013

  TAMBWE AANZA MAZOEZI KWA AJILI YA KAGERA SUGAR KESHO TAIFA

  Na Mahmoud Zubeiry, Kigamboni
  MSHAMBULIAJI Amisi Tambwe wa Simba SC aliyekosa mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Azam FC Jumatatu kutokana na maumivu ya goti, leo ameanza mazoezi mepesi kujiandaa na mchezo wa kesho dhidi ya Kagera Sugar.
  Daktari wa Simba, Yassin Gembe ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, Tambwe amefanya mazoezi mepesi leo asubuhi Bamba Beach, Kigamboni na jioni pia ataendelea.
  “Baada ya hapo tutaangalia hali yake kama ataweza kucheza kesho au la. Hatutathubutu kumlazimisha kucheza kama hajapona sawa sawa, kwa sababu ni hatari kwake na kwa timu pia,”alisema.
  Tambwe mara ya mwisho alicheza Simba na Coastal Union Tanga Jumatano iliyopita na aliwekewa ulinzi mkali na Juma Nyosso ingawa alimaliza dakika 90

  Gembe alisema kwamba tatizo kubwa ni mechi Ligi Kuu kufululiza ndiyo maana wachezaji hata wakipata maumivu kidogo inakuwa vigumu kupona haraka.   
  Simba itamenyana na Kagera Sugar kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
  Viingilio katika mechi hiyo itakayooneshwa moja kwa moja na Azam Tv kupitia TBC 1 vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 kwa VIP A.
  Nayo Yanga itashuka uwanjani Novemba Mosi mwaka huu katika mechi nyingine ya ligi hiyo dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Novemba 2 mwaka huu kutakuwa na mechi nne; Mgambo Shooting na Coastal Union (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Tanzania Prisons na Oljoro JKT (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Azam na Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), na Mtibwa Sugar na Rhino Rangers (Uwanja wa Manungu, Morogoro).
  Raundi hiyo itakamilika Novemba 3 mwaka huu kwa mechi moja ambapo Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Ashanti United kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
  Mechi za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo zitachezwa Novemba 6 na 7 mwaka huu. Novemba 6 ni JKT Ruvu vs Coastal Union, Ashani United vs Simba, Kagera Sugar vs Mgambo Shooting, Rhino Rangers vs Tanzania Prisons na Ruvu Shooting vs Mtibwa Sugar.
  Novemba 7 mwaka huu, Azam itacheza na Mbeya City wakati Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TAMBWE AANZA MAZOEZI KWA AJILI YA KAGERA SUGAR KESHO TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top