• HABARI MPYA

  Saturday, October 26, 2013

  BABU MFARANSA BADO ASOTEA CHAKE SIMBA SC, ASEMA DAR NI MAUMIVU TU KWAKE

  Na Mahmoud Zubeiry, Kariakoo
  KOCHA aliyetupiwa virago mwishoni mwa msimu, Mfaransa Patrick Liewig bado yupo nchini akisotea fedha zake, dola za Kimarekani 18,000 za malimbikizo ya mishahara yake akiwa kazini katika klabu hiyo tangu Januari hadi Mei, mwaka huu.
  Liewig aliyewasili nchini Oktoba 18, mwaka huu akitarajiwa kulipwa kutokana na mapato ya mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga iliyoingiza Sh. Milioni 500, amefikia katika hoteli ya Sapphire Court, Kariakoo, Dar es Salaam.
  Patrick Liewig kulia akiwa na Bin Zubeiry

  “Bado hadi leo sijalipwa na ninajua baada ya mechi ya Yanga walipewa fedha nyingi, ila wananifanyia kitu kibaya, naendelea kutumia fedha kulipa hoteli na kuishi hapa nikisubiri hizo fedha, naumia kwa kweli,”alisema Liewig leo.
  Liewig amesema Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Isamil Aden Rage ameahidi kukutana naye leo ili wamalizane.“Nasubiri nitakapokutana na Rage, nitajua hatima yangu, ila naumia sana, bora wanilipe nirudi zangu nyumbani kuendelea na maisha yangu mengine,” alisema.
  Juni 20, mwaka huu Simba SC ilimlipa Liewig dola za Kimarekani 10,000 kati ya dola 26,000 alizokuwa anadai klabu hiyo baada ya kumvunjia Mkataba na kuahidi kumlipa kiasi kilichobaki mwezi huu.
  Liewig alikuwa anadai malimbikizo ya mishahara ya miezi miwili, dola 12,000 na akalipwa dola 12,000 za kuvunjiwa Mkataba wakati dola 2,000 ni za tiketi yake ya kurejea kwake.
  Kocha huyo alivunjiwa Mkataba wakati amepwa likizo ya kwenda mapumzikoni kwao, baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na nafasi yake amepewa Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’.
  Hata hivyo, baada ya kurejea nchini alifanya mazungumzo na uongozi wa Simba, hatimaye wakakubaliana kulipana kwa awamu, fungu la mwisho likitarajiwa kutolewa mwezi huu.
  Liewig alisani Mkataba wa mwaka mmoja na nusu Januari mwaka huu kuifundisha Simba SC akirithi mikoba ya Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick aliyetupiwa virago.     
  Katika kipindi chake cha kuwa na klabu hiyo kwa miezi mitano, Liewig aliiongoza Simba katika mechi 25 akiiwezesha kushinda tisa, sare nane na kufungwa saba.   
  Huyu anakuwa kocha wa pili mfululizo wa kigeni Simba SC anasumbuliwa kulipwa baada ya kuvunjiwa mkataba, kwani hata Mserbia Milovan Cirkovick aliyemtangulia Liewig ilibidi alipwe na mpenzi wa klabu hiyo, Rahma Al Kharoos.    
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BABU MFARANSA BADO ASOTEA CHAKE SIMBA SC, ASEMA DAR NI MAUMIVU TU KWAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top